Wolfgang Schäuble wa CDU kuwa spika mpya wa Bundestag |
Wolfgang Schaeuble, waziri wa zamani wa fedha wa Ujerumani mwenye dhamira ya chuma, anatarajiwa kuwa spika mpya wa bunge, akisafisha njia ya mabadiliko makubwa ya madaraka katika taifa lenye uchumi mkubwa barani Ulaya.
wabunge wa Ujerumani wanafanya kikao cha kwanza cha bunge leo Jumanne, baada ya vyama vya kihafidhina vinavyoongozwa na kansela Angela Merkel kuibuka na ushindi lakini pii wakiwa hoi katika uchaguzi mkuu wa mwezi Septemba, ambao chama cha siasa kali za mrengo wa kulia kilishinda viti kwa mara ya kwanza.
Kikao cha leo kitashuhudia bunge lenye viti 709 likimchagua spika wa bunge, ambapo waziri wa fedha anyeondoka katika wadhifa huo Wolfgang Schaeuble mwenye umri wa miaka 75 , na mbunge aliyelitumikia bunge kwa muda mrefu wa miaka 45 nchini humo, akitarajiwa kuchukua nafasi ya Norbert Lammert.
Haifahamiki nani atachukua wadhifa wa makamu spika , wakati upande wa chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto cha Social Democratic SPD , ambacho kitakuwa upande wa upinzani kwa mara ya kwanza baada ya muda wa miaka minne, kikitafakari kuwateua wagombea ambao ni pamoja na kiongozi wa zamani wa kundi la wabunge wa chama hicho bungeni Thomas Oppermann na waziri wa zamani wa afya Ulla Schmidt.
Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Alernative for Germany AfD, ambacho kimepata viti 94 katika bunge hilo jipya baada ya kupata asilimia 13 ya kura, kimempendekeza Albrecht Glaser kuwa makamu wa spika.
Glaser huko nyuma amewahi kushambuliwa kutokana na taarifa za utata kuhusiana na Uislamu.
Makabiliano makali
Chama hicho cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD kinatarajiwa kukabiliana vikali na vyama vingine kutokana na uamuzi wake wa kumteua mgombea huyo wakati kikao kitakapoanza leo.
Katika kikao hicho cha leo cha Bundestag , Wolfgang Schaeuble anaweza kutarajia uungwaji mkono mkubwa na kuteuliwa kuwa spika wa bunge. Baadaye wabunge watapiga kura kuwachagua makamu sita wa spika , mmoja kutoka kila chama kinachowakilishwa bungeni.
Uteuzi wa makamu wa spika wa chama cha AfD , ambae ni Albrecht Glaser , mwenye umri wa miaka 75, unaleta utata baada ya kiongozi huyo kutoa maelezo ya kuukashifu Uislamu kwamba ni nadharia ya kisiasa badala ya dini , na kusema Waislamu hawapaswi kupewa haki ya uhuru wa kidini kwa kuwa Uislamu hauheshimu uhuru huo.
Chama cha Social Democrats , SPD, kile cha Kijani , Greens, chama kinachopendelea wafanyabiashara cha Free Democrats FDP na kile kinachoelemea zaidi siasa kali za mrengo wa kushoto cha Left Party vimezungumzia kupinga uteuzi wa Glaser.
Andrea Nahles , kiongozi wa chama cha Social democrats bungeni , amekiambia kituo cha televisheni cha ZDF kwamba glaser ameshindwa kusahihisha matamshi yake kuhusu Uislamu, hali inayokwenda kinyume na haki ya uhuru wa kuabudu nchini Ujerumani, na kutupilia mbali ombi lake la kutaka mjadala kuwa ni kichekesho.
@habari na Dw swahil
No comments:
Post a Comment