Wednesday, 8 November 2017

Rais Magufuli afafanua deni la Taifa.


Dar es Salaam.
 Wakati deni la Taifa likitajwa kuongezeka, Rais John Magufuli amesema hali hiyo isiwashangaze Watanzania.

Amesema madeni hayo yanaonyesha imani ya mataifa makubwa kwa Tanzania kuhusu uwezo wa kuyalipa.
Rais Magufuli amesema kiwango cha mikopo ni kidogo ikilinganishwa na mataifa mengine ya Afrika.
Akizungumza leo Jumatano Novemba 8,2017 na wananchi wa Missenyi mkoani Kagera alikotembelea kiwanda cha sukari  Kagera, Rais Magufuli amesema kiwango kilichofikiwa ni cha kawaida.
Akiwasilisha bungeni jana Jumanne Novemba 7,2017 mapendekezo ya mpango wa maendeleo ya Taifa na mwongozo wa mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2018/19, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema deni limeongezeka kwa asilimia 17.
Dk Mpango alisema miradi mitano ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa na serikali imechangia ongezeko la asilimia 17 ya deni la Taifa ambalo ni zaidi ya Dola 26.115 bilioni za Marekani (zaidi ya Sh57.453 trilioni).
“Ongezeko hilo linachangiwa na mikopo mipya iliyochukuliwa ili kugharamia miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), Strategic Cities, Mradi wa Usafirishaji Dar es Salaam (Dart) na kupanua upatikanaji wa maji safi Dar es Salaam,” alisema.Rais Magufuli akizungumza na wananchi wa Missenyi amesema kuongezeka kwa deni hilo kunatokana na baadhi ya mikopo iliyodumu kwa muda tangu awamu zilizopita.
“Watu wanasema Serikali inakopakopa sana. Tajiri yeyote lazima akope na ukishakopa maana yake unaheshimika. Mtu ambaye hawezi kukopesheka ina maana haaminiki,” amesema.
Amesema, “Kukopa na kuwa na madeni si dhambi. Madeni mengine tunahangaika nayo leo hii yalikopwa tangu enzi za Mwalimu Nyerere,” amesema.
Rais Magufuli amesema suala la msingi ni kuangalia ni namna gani fedha hizo zinavyotumika.
Amesema fedha zilizokopwa zimeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara na reli.
@chanzo mwananchi

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...