Saturday, 11 November 2017

Songwe yaongoza kwa kipindupindu.





Dar es Salaam.
 Wizara ya Afya imesema  watu 18 wamefariki kwa ugonjwa wa kipindupindu katika mikoa kadhaa nchini kuanzia Septemba mosi mpaka Oktoba 30.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara hiyo leo Novemba 11, kwa vyombo vya habari limesema mpaka sasa kuna wagonjwa  570.
Taarifa hiyo imesema kwamba mkoa wa Songwe  unaongoza kwa kuwa na wagonjwa  wengi ukifuatiwa na Mkoa wa Mbeya. Mikoa mingine ambayo imeathirika kwa ugonjwa huo ni Tanga, Iringa, Kigoma, Dodoma na  Morogoro.
Katika kukabiliana na ugonjwa huo wizara imetoa tahadhari na kuzidisha juhudi za kuzuia , kwa kusimamia kikamilifu maelekezo na miongozo stahiki inayotolewa.
‘’Tunalekea kwenye kipindi cha  mvua ambazo zinaweza kuongeza kuenea kwa maambukizo ya ugonjwa huu na mengine mengi hivyo ni vizuri ikachukuliwa tahadhari mapema ’’ imesema sehemu ya taarifa hiyo. 
Timu ya ufuatiliaji wa ugonjwa wa kipindupindu imebaini kuwa wagonjwa wamekuwa wakiishi mbali na kituo cha afya hali ambayo inasababisha  wagonjwa kukosa huduma za afya kwa wakati na  kusababisha  kupoteza maisha.
Wizara kupitia taarifa yake imeagiza kuwapo kwa  vituo vya kutolea “Oral Rehydration Salt”, maarufu kama ORS, vianzishwe na halmashauri kwa kushirikiana na jamii ili kuzuia vifo.
 “Endapo ORS haitapatikana, jamii ielekezwe kuchanganya chumvi na sukari kwa kutumia maji safi yaliyochemshwa kiasi cha lita moja na vijiko viwili vya sukari na nusu kijiko ya chumvi’’ imesema sehemu ya taarifa na kuongeza  
‘’ Njia hii ya kutumia ORS au mchanganyiko wa chumvi na sukari ndio njia  muhimu ya kuokoa maisha ya mgonjwa wa kipindupindu kwani inasaidia kupunguza kasi ya kupungukiwa kwa maji mwilini inayosababisha kifo,” imesema
Taarifa inasema  kuwa ushirikishwaji wa sekta zote kwa ngazi zote hadi katika jamii ni muhimu sana katika kukabiliana na ugonjwa wa Kipindupindu. 
Hata hivyo Wizara inasisitiza kuwa wadau wote wapewe nafasi katika mapambano haya kupitia vikao mbalimbali ili kujadili udhibiti wa ugonjwa wa Kipindupindu kwenye halmashauri na mikoa.
Viongozi wa dini, watu mashuhuri na waganga wa tiba mbadala pia wasaidie kuhamasisha jamii zao kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu.
Wizara inaendelea kuwasihi wananchi kuungana na Halmashauri, mikoa pamoja na wizara katika juhudi za kupambana na kuenea kwa ugonjwa wa Kipindupindu.
 Chanzo:mwananchi

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...