Sunday, 21 January 2018

Wajumbe wa SPD kuamua juu ya muungano na Angela Merkel.



Deutschland Außerordentlicher SPD-Parteitag in Bonn Martin Schulz (picture-alliance/dpa/K. Nietfeld)
Chama cha kisoshalisti cha SPD, Jumapili hii kitaamua juu ya kuanza mazungumzo ya kuunda muungano na wahafidhina wa kansela Angela Merkel, hatua itakayoisogeza mbele Ujerumani katika kupata serikali imara.
Mwenyekiti wa SPD Martin Schulz anakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa makundi ya vijana na lile la msimamo mkali wa mrengo wa kushoto, ambayo yanahoji kuwa chama cha SPD kinapaswa kujijenga upya kikiwa upande wa upinzani baada ya kupata matokeo mabaya zaidi ya uchaguzi mwezi Septemba, tangu Ujerumani ilipogeuka Jamhuri ya Shirikisho mwaka 1949.
Karibu wajumbe 600 wanaokutana mjini Bonn, watajadili na kupiga kura juu ya iwapo viongozi wao wanapaswa kuendelea na majadiliano ya kuendeleza muungano na wahafidhina wa Merkel, wa tawala ulioingia madarakani mwaka 2013.
Pande hizo mbilo, ambazo zote zilipoteza uungwaji mkono kwa chama cha siasa kali za mrengo mkali wa kulia cha AfD katika uchaguzi wa Septemba 24, zilifikia makubaliano ya awali wiki iliyopita lakini wakosoaji, akiwemo kiongozi wa tawi la vijana la chama cha SPD Kevin Kuehnert, wanasema makubaliano yaliofikiwa hayajajumuisha masuala ya kutosha yanayosimamia SPD.
Deutschland Nachwuchspolitiker aktuell & historisch | Kevin Kühnert, SPD 2018 (Imago/R. Zensen)
Kiongozi wa tawi la vijana wa SPD Kevin Kuenert, ameibuka kuwa kiongozi wa vuguvugu linalopinga kushiriki tena kwa chama hicho katik serikali ya muungano mkuu (GraKo).
Kura hiyo ya Jumapili itafuatiliwa kwa karibu pia na mataifa ya nje kwa kuzingatia ukweli kwamba Ujerumani ndiyo taifa kubwa zaidi kiuchumi barani Ulaya na Merkel amebeba jukumu la uongozi kwa muda mrefu, katika masuala ya kiuchumi na kiusalama barani humo.
Wanachama waandamizi wa SPD wameelezea kupiga hatua katika kutafuta uungwaji mkono kwa ajili ya kuanzisha mazungumzo rasmi, baada ya tawi kubwa zaidi la kijimbo la SPD, la North Rhine-Westphalia (NRW) kuwapendekezea wanachama wake kupiga kura ya kuunga mkono majadiliano - kwa sharti kwamba Schulz anashinikiza muafaka zaidi kuhusu sera za ajira, afya na uhamiaji.
Kiongozi wa wabunge wa SPD Andrea Nahles alisema anatarajia mazungumzo rasmi kufanyika. "Pamoja na hayo, namuomba kila mmoja katika chama changu kuwajibika. Tafadhali zingatieni madhara ikiwa juhudi za kuunda serikali hii zitashindwa," aliliambia gazeti la Welt am Sonntag.
Mkwamo
Kura ya hapana ndani ya SPD itasababisha kipindi kirefu cha mkwamo wa kisiasa, mnamo wakati uchumi wa Ujerumani unazalisha ziada za kibejti, na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anaitegemea Berlin kuungana naye kuufanyia mageuzi Umoja wa Ulaya kufuatia uamuzi wa Uingereza kujiondoa katika umoja huo.
Mambo yanayoweza kutokea ikiwa wajumbe wa SPD watakataa majadiliano yanahusisha kuitishwa uchaguzi mpya au kuunda serikali ya wachache kwa kile kitakachokuwa mara ya kwanza katika historia ya Ujerumani ya baada ya vita.
Sitzung der SPD-Bundestagfraktion - Andrea Nahles (picture alliance/dpa/B. von Jutrczenka)
Kiongozi wa wabunge wa SPD Andrea Nahles.
Kiongozi wa SPD katika jimbo la North Rheine-Westphalia Michael Groschek, alisema mwishoni mwa wiki kuwa yeye pia alitarajia matokeo ya chanya, ingawa makubaliano ya mwisho ya kuunda muungano, yatatakiwa bila shaka kutofautiana na kilichopo kwenye karatasi.
Tawi la SPD katika jimbo hilo linataka makubaliano ya mwisho ya kuunda serikali yahusishe wito wa kufuta mfumo wa Ujerumani wa bima mbili za afya - ya umma na ya binafsi na kuundwa mfumo mmoja wa kiraia, ili kupunguza mikataba ya ajira za muda na kuruhusu kuungana kwa familia za waomba hifadhi wanaokabiliwa na ugumu usiyo wa kawaida.
Sharti za kuwepo na tahfifu zaidi lilikatiliwa mara moja na wahafidhina, huku vyama vya wafanyabiashara wakiwataka wajumbe wa SPD kuunga mkono majadiliano ya kuunda serikali, wakisema hatua ya kukataa inaweza kuitumbukiza nchi hiyo katika mgogoro mbaya kabisaa wa kisiasa.
Mkutano huo maalumu wa SPD siyo kihunzi cha mwisho hata hivyo. Wanachama wote watapata fursa ya kuyapigia kura makubaliano ya mwisho, ikiwa yatakuwepo.
Chanzo:Dw swahili

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...