Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema haijulikani ni lini wataweza kuyamaliza mazungumzo ya kuunda serikali mpya ya mseto kati ya vyama vya kihafidhina CDU/CSU na SPD.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema chama chake cha kihafidhina cha Christian Democratic Union CDU na chama ndugu cha Christian Social Union CSU vinafanya mazungumzo magumu na chama cha Social Democrats- SPD, vikijaribu kuunda serikali mpya ya mseto miezi minne baada ya uchaguzi mkuu. Merkel amesema haijulikani ni lini wataweza kuyamaliza mazungumzo hayo.
Kushindwa mpaka sasa kuundwa kwa serikali mpya ya mseto kati ya CDU/CSU na SPD kumesababisha wasiwasi miongoni mwa wawekezaji na nchi washirika ambao wanategemea Ujerumani kuweza kuwa na usemi zaidi katika masuala yanayoukabili Umoja wa Ulaya kama mchakato wa kujiondoa kwa Uingereza kutoka umoja huo, mchakato ujulikanao kama Brexit na pia kuyasogeza mbele mageuzi kuhusu sera zinazohusu kanda inayotumia sarafu ya euro.
Haijulikani mazungumzo yatakamilika lini
Vyama hivyo vya kihafidhina na SPD vilikuwa vimejiwekea Jumapili (04.02.2018) kuwa muda wa mwisho wa kufikia makubaliano ya kuunda serikali ya mseto kama ambayo imeongoza tangu 2013 lakini baadhi ya wanasiasa wa pande zote wamesema huenda mazungumzo hayo yakaendelea hadi Jumatatu au Jumanne na zaidi ya hayo, wanachama wa wote wa SPD wanapaswa kuridhia kwanza makubaliano yaliyofikiwa katika mazungumzo hayo.
Kabla ya kuelekea katika mazungumzo hayo, Merkel ambaye amekuwa madarakani kama Kansela wa Ujerumani kwa miaka 12, amesema haiwezekani bado kusema mazungumzo hayo yatadumu kwa muda gani licha ya kuwa siku ya Jumamosi walifikia mengi lakini bado kuna masuala muhimu ambayo yanahitaji kutatuliwa.
Vyama hivyo vilikubaliana kuhusu nishati na kilimo siku ya Jumamosi lakini bado viongozi wanaendelea kuvutana kuhusu suala la afya. Merkel ambaye anaitegemea SPD kumuwezesha kuongoza rasmi muhula wake wa nne madarakani amesema anaelekea kwenye mazungumzo ya Jumapili kwa nia njema lakini anatarajia mazungumzo hayo kuwa magumu.
Kiongozi wa SPD Martin Schulz amesema pande zote mbili zimekubaliana kuhusu masuala mengi katika kipindi cha siku za hivi karibuni lakini bado wanatofautiana juu ya matakwa ya chama chake cha kufutilia mbali mikataba ya muda mfupi kwa wafanyakazi na kutaka mageuzi katika bima ya afya. Schulz ameongeza kusema itabidi wajadiliane kwa kina kuhusu masuala hayo na anatumai makubaliano yatafikiwa.
Bado kuna masuala yanayozua utata
Wahafidhina wanapinga wito wa SPD wa kuwepo mageuzi makubwa kuhusu bima ya afya na sasa mazungumzo yanatarajiwa kuangazia kuboresha huduma za afya ya umma kwa kubadilisha sheria za jinsi madakatari wanavyowahudumia wagonjwa walio na bima ya kampuni binafsi za kutoa huduma za bima.
CDU na CSU pia havitaki kuondolewa kwa mikataba mifupi ya ajira lakini vimependekeza kuzuia mikataba kama hiyo katika siku za usoni ili kujaribu kufikia muafaka na SPD.
Duru zilizo karibu na mazungumzo hayo zimearifu kuwa vyama vyote vimekubaliana kuhusu suala la kodi za nyumba na ujenzi wa nyumba kwa wenye uwezo mdogo, suala ambalo pia lilikuwa likileta mivutano lakini makubaliano hayo yatahitaji kwanza kuidhinishwa na wajumbe wakuu wanaosimamia mazungumzo hayo.
Schulz amesema anataka kuona mazungumzo yakisonga kwa mwendo wa kasi lakini ameonya kuwa vyama visijiweke katika shinikizo la kukimbizana na muda kwani haitakuwa na manufaa katika hatua ya mwisho ya mazungumzo hayo.
Kiongozi huyo wa SPD ameongeza kuwa kuna haja ya kuchukua muda kuweka misingi thabiti ya kuwepo serikali thabiti. Mazungumzo hayo ya Jumapili yanatarajiwa kuendelea hadi usiku.
Kila upande unasitasita kuridhia matakwa zaidi ya upande mwingine, lakini pia pande zote hizo zinahofu kuingia katika uchaguzi mpya, ambao vinahisi unaweza kukipa nguvu zaidi chama chenye sera kali za mrengo wa kulia, Alternative für Deutschland- AfD.
Chanzo: Dw swahili
#Changia Damu Okoa Taifa
No comments:
Post a Comment