Ripoti ya waangalizi huru wa Umoja wa Mataifa imebainisha kuwa Korea Kaskazini ilipata takriban dola milioni mia mbili mwaka uliopita kutokana na uuzaji wa bidhaa zilizopigwa marufuku katika mataifa ya nje huku ikikiuka vikwazo ilivyowekewa na jamii ya kimataifa.
Ripoti hiyo iliyovuja kutoka kwa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imesema kuwa nchi kadhaa zikiwemo, China, Urusi na Malaysia zilishindwa kuzuia uuzaji huo.
Inasemekana Korea Kaskazini ilituma shehena ya silaha hadi nchini Syria na Myanmar huku ikikiuka vikwazo hivyo vya Umoja wa Mataifa.
Waangalizi hao pia walichunguza shehena ya mkaa iliyosafirishwa na meli ishirini hadi nchi jirani.
Balozi wa Myanmar katika Umoja wa Mataifa amesema taifa lake halina mkataba wowote wa silaha na Korea Kaskazini.
Aidha ripoti hiyo imenadi kuwa kampuni kadhaa za kimataifa za mafuta zilihusika kuiuzia Korea Kaskazini bidhaa zao.
Vikwazo vipya vya Umoja wa Mataifa vilivyotangazwa mwezi Disemba vilikadiriwa kupunguza ununuzi wa mafuta katika taifa hilo kwa asilimia 90 .
Vilishirikisha marufuku za bidhaa inazouza nje kama vile mashine na viufaa vya kielektroniki.
Wakati huohuo raia wote wa Korea Kaskazini wanaofanya kazi katika mataifa ya kigeni waliagizwa kurudi nyumbani katika kipindi cha miezi 24.
Wachunguzi wa UN walibaini kwamba Myanmar na Syria zimekuwa zikishirikiana na Korea Kaskazini katika ununuzi wa silaha, Komid licha ya silaha hiyo kuorodheshwa katika vikwazo vya Umoja wa Mataifa.
Ripoti hiyo imesema kuwa kuna ushahidi kwamba Korea Kaskazini ilikuwa ikisaidia Syria kutengeza silaha za kemikali mbali na kuiuzia Myanmar silaha za masafa marefu.
Vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni vimekuwa vikilenga biashara ya mkaa na China, bidhaa za kuuza nje zilizopigwa marufuku, vikwazo vya kusafiri, mali za watu binafsi na kampuni zinazohusishwa na mpango wa kinyuklia.
Chanzo:Bbc swahili
#Changia Damu Okoa Taifa
No comments:
Post a Comment