Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma |
Makubaliano hayo ndiyo yaliyosababisha kuahirishwa kwa mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa chama tawala cha African National Congress (ANC) uliopangwa kufanyika Jumatano ili kulazimisha Zuma kuondoka ofisini.
Mkutano huo ulikuwa umepangwa kufanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Mount Nelson mjini Cape Town na ungepokea mapendekezo kutoka Kamati Kuu ya Taifa ya ANC kwamba Zuma aondolewe kama mkuu wa nchi.
Mkutano kati ya Zuma na Ramaphosa ulifanyika baada ya Spika wa Bunge, Baleka Mbete kutangaza kuahirishwa kwa hotuba ya kitaifa iliyokuwa itolewe na Zuma Alhamisi.
Zuma alitumia Jumanne asubuhi akifanya vikao na kamati za Baraza la Mawaziri mjini Tuynhuys. Baadaye, alikwenda Genadendal yaliko makazi yake ya kifahari huko Cape Town ambako alikutana na Ramaphosa baada ya saa 10:00 jioni pamoja na Katibu Mkuu wa ANC, Ace Magashule.
Januari 6, 2018, Mbete alitangaza kuahirishwa kwa muda usiojulikana kwa hotuba ya hali ya nchi maarufu kama Sona iliyokuwa itolewe na Zuma.
Jumanne jioni, Magashule aliiambia TimesLIVE kuwa mkutano kati ya marais wawili ulikuwa "wa kujenga na wenye mafanikio".
"Nilikuwa huko ... niliwaacha marais wawili hao kujadili mambo yao mimi nilirudi kuungana nao mwishoni," alisema.
Magashule alisema Zuma na Ramaphosa walikubaliana kuwa uamuzi wa kuahirishwa hotuba ya rais ulikuwa sahihi.
"Walikubaliana pia kuwa mkutano wa dharura wa NEC ulioitishwa unapaswa kuahirishwa baada ya majadiliano yao yenye kujenga," alisema.
Magashule hakutaka kuthibitisha ikiwa Zuma amekubali kujiuzulu, ingawa viongozi wengine wa ANC walidokeza kuwa mpango uliokubaliwa utamwezesha Zuma "kuondoka kwa njia ya heshima".
Hata hivyo alidokeza kwamba majadiliano kati ya Ramaphosa na Zuma yaliridhia haja kubwa ya NEC kujadili kuondoka kwake.
Katibu mkuu huyo hakuweza kusema nani atatoa hotuba mara tarehe mpya itakapotangazwa.
Chanzo:Mwananchi
#Changia Damu Okoa Taifa
No comments:
Post a Comment