Rais John Magufuli ameeleza sababu za kuteuwa baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, ambapo hadi sasa amewateuwa viongozi wawili kutoka chama cha ACT-Wazalendo, akiwemo Mwenyekiti Taifa wa chama hicho, Anna Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Baada ya kumuapisha Mama Mghwira Juni 6,2017 Ikulu jijini Dar es Salaam, Dkt. Magufuli amesema hateuwi watu wanaopiga kelele na kupinga jitihada za serikali, bali huteua watu wenye utayari wa kufanya kazi kwa ajili ya kutumikia watanzania.
“Wapo watu kila kitu ni kupinga tu, siteui watu wanao pigapiga kelele, nateua mtu ambaye ninajua nikimpeleka mahali atafanya kazi kwa niaba ya watanzania,” amesema.
Pia, Rais Magufuli amesema ameteuwa viongozi wa vyama vya upinzani kushika nyadhifa serikalini kwa sababu anataka upinzani uwepo katika serikali yake.
“Pamoja kwamba wapo wengi wana niomba niwachague, mpaka wabunge nikasema hapana nataka upinzani uwepo,” amesema.
Kuhusu RC Mghwira, amemtaka akafanye kazi ya kutatua shida za watanzania, huku akimtaka kutosikiliza maneno ya watu kwani wivu wa kutoteuliwa ndio unaosababisha baadhi ya watu kusema kuhusu uteuzi wake.
“Nenda ukafanye kazi katumikie watanzania kamtangulize Mungu kafanye kazi ya Mungu kwa ajili ya watanzania, katatue shida za watanzania, kusemwa utasemwa tu, umeshaingia humu sasa wengine wanakuonea wivu, wapo wanaokuonea wivu kwenye chama chako, na hata CCM walitaka nichague tu kutoka kwao, hata wa Chadema watakuonea wivu sababu sikuchagua huko,” amesema.
Kwa upande wake RC Mghwira amemuahidi Rais Magufuli kufanya kazi kwa bidi ili kusimamia shughuli za maendeleo kwa kuwa hakuna chama kinachopinga maendeleo.
“Ninaamini kazi za mkuu wa mkoa ni kusimamia shughuli za maendeleo kwenye mkoa sijui kama kipo chama kinachopinga maendeleo ya kila eneo la nchi yetu na nje ya nchi ya mipaka yetu,” amesema Mama Mghwira.
Pamoja na RC Mghwira, Rais Magufuli mwezi Aprili mwaka huu alimteua aliyekuwa Mshauri Mkuu wa ACT-Wazalendo, Profesa Kitila Mkumbo kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
No comments:
Post a Comment