Monday, 28 August 2017

Kimbunga Harvey: Watu 2,000 waokolewa kutoka kwa mafuriko Houston, Marekani

Maeneo yaliyoathirika na mafuliko
Watu takriban 2,000 wameokolewa kutoka kwa mafuriko katika mji wa Houston na viunga vyake, huku kimbunga Harvey kikiendelea kusababisha mvua kubwa sana maeneo ya jimbo la Texas.
Kumekuwa na ripoti za kutokea kwa vifo pamoja na magari kadha kuzidiwa na nguvu za maji.
Hata hivyo, uchunguzi bado unaendelea, afisi ya liwali mkuu wa wilaya ya Harris, Darryl Coleman amesema.
Gavana wa Texas Greg Abbott ameambia wanahabari kwamba hawezi kuthibitisha vifo vinavyodaiwa kutokana na mafuriko hayo.
Idara ya Taifa ya Hali ya Hewa (NWS) imesema hali ambayo inashuhudiwa katika eneo hilo haijawahi kushuhudiwa awali.
Idara hiyo imesema kulitokea mafuriko ya ghafla eneo la katikati mwa mji wa Houston, na uchukuzi umetatizika.
Vyumba vingi vya kutoa hifadhi wakati wa majanga vimefunguliwa, ukiwemo ukumbi mmoja wa mikutano.
Gavana Abbot amesema barabara karibu 250 zimefungwa Texas na kwamba ameiomba serikali kuu itangaze janga katika wilaya 19, ombi ambalo limeidhinishwa na Rais Donald Trump.
"Tutaendelea kupokea mvua kubwa," amesema gavana huyo.



NWS awali walisema walikuwa wamepokea taarifa za vifo vitano, lakini wamesema wameweza kuthibitisha kifo cha mtu mmoja pekee eneo la Houston.
Kufikia sasa, watu wawili wamethibitishwa kufariki tangu kimbunga hicho kilichofika maeneo ya bara, katika wilaya ya Aransas, ambapo Rockport ndio mji mkuu, mtu mmoja alifariki baada ya nyumba yake kushika moto Ijumaa usiku.
Na eneo la Houston, mwanamke mmoja alifariki akiendesha gari katika barabara zilizokuwa zimefurika maji Jumamosi.
Meya wa Houston Sylvester Turner amewashauri wakazi kutopigia simu maafisa wa huduma za dharura ila tu iwapo maisha yao yanatishiwa na wanahitaji kuokolewa kwa dharura.
"Msiingie barabarani. Msifikirie kwamba kimbunga kimepita," amesema.
Mjini Washington, ikulu ya White House imesema Rais Trump atazuru Texas Jumanne kutathmini uharibifu uliosababishwa na kimbunga hicho.

Rais Trump alikuwa amesema awali kwamba angezuru eneo hilo haraka iwezekanavyo lakini kwa kuhakikisha kwamba hatatatiza juhudi za uokoaji.

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...