Tuesday, 29 August 2017

MBUNGE WATUNDUMA AKAMATWA NA POLISI LEO.


Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka 
Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka amekamatwa na polisi akiwa katika viwanja vya Mahakama ya Wilaya ya Mbozi mjini Vwawa.

Mwakajoka amekamatwa leo Agosti 29 baada ya kufika mahakamani hapo kufuatilia kesi inayomkabili mbunge mwenzake wa Mbozi, Pascal Haonga.
Katibu wa Chadema Wilaya ya Mbozi, James Mbasha amesema mbunge huyo amekamatwa lakini hajui kosa linalomkabili.
Mbasha amesema alipata taarifa leo asubuhi kwamba mbunge huyo anatafutwa na polisi.
Katika kesi mahakamani hapo, Haonga na wenzake wawili Wilfred Mwalusanya na Mashaka Mwampashi wanakabiliwa na mashtaka mawili, kufanya vurugu na kuwazuia askari kufanya kazi yao kinyume cha sheria.
Mwendesha mashitaka wa polisi, Samwel Saro anadai jana Agosti 28 saa saba mchana, washtakiwa walimzuia askari kutimiza majukumu yake ya kumkamata Mwampashi aliyedaiwa kwamba si mjumbe halali katika uchaguzi wa mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mlowo.
Washtakiwa pia wanadaiwa kumfanyia vurugu msimamizi wa uchaguzi huo ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mbozi,  Lauteri Kanoni.
Washitakiwa walikana mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo,  Asha Waziri ambaye alisema dhamana iko wazi kwa kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho kutoka kwa watendaji wa maeneo yao watakaoweka bondi ya Sh2 milioni kila mmoja.


Washtakiwa walitimiza masharti na kuachiwa huru kwa dhamana. Kesi itatajwa Septemba 25 na washtakiwa watasomewa maelezo ya awali.

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...