Tuesday, 19 September 2017

Suu Kyi: Tunalaani ghasia dhidi ya Rohingya


Myanmar Aung San Suu Kyi (Getty Images/AFP/Ye Aung Thu)
Kiongozi wa Myanmar, Aung San Suu Kyi amelihutubia taifa ambapo amezungumzia ghasia zinazoendelea nchini humo dhidi ya Waislamu wa Rohingya katika jimbo la Rakhine.
Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu kuzuka kwa ghasia hizo mwezi uliopita, Aung San Suu Kyi amesema serikali yake inalaani vikali ukiukwaji wa haki za binaadamu na unyanyasaji unaofanywa kinyume cha sheria. Amesema wako tayari kuanza mchakato wa kuwarejesha nyumbani wakimbizi wowote ambao wanataka kurejea nchini humo baada ya kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh.
Suu Kyi mwenye umri wa miaka 72, na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel ameitoa hotuba hiyo baada ya mataifa yenye nguvu duniani kuionya Myanmar kwamba inaweza ikakabiliwa na hatua, iwapo haitachukua hatua za kukomesha ukandamizaji unaofanywa dhidi ya jamii ya watu wachache wa Rohingya katika jimbo la Rakhine.
Kiongozi huyo wa Myanmar amesema wana wasiwasi kuhusu Waislamu wanaokimbilia Bangladesh ambapo idadi yao ni 400,000. Ameahidi kuchukua hatua dhidi ya mtu yeyote aliyevunja sheria na kukiuka haki za binaadamu, lakini amesisitiza kuwa vijiji vingi vya Waislamu wa Rohingya havijaathirika na ghasia hizo na amewaalika wanadiplomasia wa kigeni kulizuru jimbo la Rakhine.
Bangladesch Tankhali Rohingya Flüchtlinge (Getty Images/P. Bronstein)
Wakimbizi wa Myanmar wakigombania chakula na nguo Bangladesh
''Tunawaalika kujumuika nasi, kuzungumza nasi, kwenda nasi katika maeneo yaliyoathirika, kujionea wenyewe kile kinachoendelea. Na kuangalia kile ambacho tunaweza kufanya kwa pamoja kuondoa matatizo haya. Pia nataka muyaangalie kwa umakini maeneo yenye amani na jinsi gani wameweza kuilinda hiyo amani,'' alisema Suu Kyi.
Tutaumaliza mzozo haraka iwezekanavyo
Suu Kyi amesema anasikitishwa na mateso wanayokumbana nao raia katika mzozo huo na anataka kuyamaliza mateso hayo haraka iwezekanavyo. Amesema Myanmar haikuwa na hofu ya uchunguzi wa kimataifa, lakini ameomba msaada wa kutafuta suluhisho la kudumu la mzozo huo na kwamba serikali yake inafanya juhudi za kuimarisha amani na utulivu.
Kamishna wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia haki za binaadamu, Zeid Ra'ad Al Hussein amesema hali ya Rohingya inaonekana kuwa kama mfano wa safisha safisha ya kikabila.
Wakati huo huo, shirika la kimataifa la haki za binaadamu, Amnesty International limemkosoa Suu Kyi na serikali yake ikisema kuwa ''inazika kichwa chake kwenye mchanga'', ikimaanisha kuyafumbia macho matatizo, kutokana na kushindwa kuchukua hatua kukabiliana na ghasia zinazoendelea Rakhine. Shirika hilo limesema kuna ushahidi mkubwa kwamba vikosi vya usalama vilihusika katika kampeni ya safisha safisha ya kikabila.
Wakati hayo yakijiri, wachunguzi wa kimataifa wa haki za binaadamu wamesema leo kuwa wanahitaji kupata ruhusa kuchunguza mzozo huo unaoendelea Myanmar, huku wakiisihi serikali kutafakari upya hatua ya kukataa kufanyika uchunguzi. Mwenyekiti wa tume ya uchunguzi, Marzuki Darusman ameliomba Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa muda zaidi wa kuchunguza madai ya kuwepo mauaji ya watu wengi, mateso, unyanyasaji wa kingono, matumizi ya mabomu ya kutegwa ardhini pamoja na uchomwaji wa vijiji.
@habari na Dw swahili

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...