picha ya wabunge wapya wakiapa leo |
Wabunge wapya wa Viti Maalum wa Chama cha Wananchi CUF
wakila kiapo cha utii bungeni baada ya kuanza kwa kikao cha kwanza cha Mkutano
wa Nane wa Bunge mjini Dodoma leo. Waliopo Juu kuanzia kushoto ni Alfredina
Kahigi, Kiza Hussein Mayeye, Nuru Awadh Bafadhili, Rukia Ahmed Kassim na
waliopo chini kuanzia kushoto ni Shamsia Aziz Mtamba, Sonia Jumaa Magongo na
Zainab Mndolwa Amir. Picha na Edwin Mjwahuzi
Wabunge hao wapya wanachukua nafasi ya wengine wanane wa CUF
waliovuliwa uanachama.
Dodoma. Kambi ya Upinzani Bungeni imesusia kuapishwa kwa
wabunge saba wa Viti Maalumu kutoka Chama cha CUF.
Wabunge hao wameapishwa leo Septemba 5 na Spika wa Bunge,
Job Ndugai.
Wakati wabunge hao wakitoka ndani ya ukumbi wa Bunge,
waliobaki kushuhudia ni wabunge wa CUF, Magdalena Sakaya (Kaliua), Maftah
Nachuma (Mtwara Mjini) na Maulid Mtulia (Kinondoni).
Awali, wafuasi wa CUF walifika asubuhi katika viwanja vya
Bunge kushuhudia kuapishwa kwa wabunge hao walioteuliwa hivi karibuni na Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
Wafuasi hao waliambatana na Mbunge wa Bunge la Afrika
Mashariki, Habib Mnyaa walifika wakiwa kwenye magari matatu aina ya Toyota
Coaster na mengine madogo yaliyokuwa yamebandikwa picha za Mwenyekiti wa CUF,
Profesa Ibrahim Lipumba, anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
Wabunge wa Viti Maalumu waliapishwa leo ni Alfredina Kaigi,
Kiza Mayeye, Nuru Bafadhili, Rukia Kassim, Shamsia Mtamba, Sonia Magogo na
Zainab Amir.
Hindu Mwenda, ambaye angeapishwa leo alifariki dunia Ijumaa
Septemba Mosi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kuzikwa Jumapili
Septemba 3.
No comments:
Post a Comment