Spika wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Pius Msekwa |
Msekwa, ambaye pia alikuwa makamu
mwenyekitiwa CCM, ametoa kauli hiyo wakati akizungumza kwa njia ya simu na gazeti
hili kuhusu hatua ya Mahakama Kuu ya Kenya kubatilisha uchaguzi wa rais wa nchi
hiyo uliofanyika Agosti 8 baada ya mgombea wa upinzani kufungua kesi, akidai
kulikuwa na ukiukwaji wa sheria.
Spika wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Pius Msekwa
amesema wakati wa kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais mahakamani umeshafika na
kilichobaki ni kupitisha rasimu ya Katiba ambayo ina ibara inayotoa haki hiyo.
Msekwa, ambaye pia alikuwa makamu mwenyekitiwa CCM, ametoa
kauli hiyo wakati akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili kuhusu hatua ya
Mahakama Kuu ya Kenya kubatilisha uchaguzi wa rais wa nchi hiyo uliofanyika
Agosti 8 baada ya mgombea wa upinzani kufungua kesi, akidai kulikuwa na
ukiukwaji wa sheria.
Kwa uamuzi huo, ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta, anayewania
kuongoza taifa hilo kwa kipindi cha pili mfululizo, umebatilishwa na sasa
atapambana tena na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga wa muungano wa NASA.
Wakati ibara ya 140 ya katiba ya Kenya inaruhusu mtu yeyote
kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais mahakamani ndani ya siku saba tangu
kutangazwa kwa mshindi, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakataza.
Ibara ya 74(12) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
inasema hakuna mahakama yoyote nchini itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza
jambo lolote lililotendwa na Tume ya Uchaguzi (NEC) katika kutekeleza madaraka
yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba.
Hilo ni jambo ambalo limekuwa likijadiliwa tangu
kubatilishwa kwa uchaguzi wa rais wa Kenya, lakini alipoulizwa kuhusu suala
hilo, Msekwa muda umefika.
“Jibu ni ndiyo,” alisema Msekwa.
“Tunaweza kufikia hatua hiyo na tumeshaifikia. Katiba Mpya
iliyopitishwa na Bunge mwaka 2014 inasema matokeo ya urais yanaweza kupingwa
mahakamani.
“Katiba ya sasa hairuhusu, lakini katiba inayopendekezwa
imeruhusu. Tunachosubiri ni referendum (kura ya maoni) tu.”
Mchakato wa kubadili Katiba ulianzishwa na Rais wa Serikali
ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete mwishoni mwa mwaka 2011 lakini ukakwama mwaka
2014 ukiwa katika hatua ya kura ya maoni baada ya NEC kueleza kuwa haikuwa na
muda wa kutosha .
Hata hivyo, mchakato huo uliingiwa na dosari baada ya baadhi
ya wajumbe wa Bunge la Katiba, hasa kutoka vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF
na NLD kuususia wakidai kuwa chombo hicho kiliacha Rasimu ya Katiba
iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuingiza ajenda za chama
tawala.
Hata hivyo, wajumbe waliosalia waliendelea na mchakato na
kupitisha Katiba Inayopendekezwa.
Hata hivyo, Rais John Magufuli ameshasema kuwa Katiba mpya
si kipaumbele chake kwa kuwa kwa sasa anataka “kuinyoosha nchi”.
Kuhusu suala hilo, Msekwa alisema hawezi kuzungumzia utawala
wa sasa kwa kuwa una utendaji wake.
“Mambo ya utawala wa sasa siwezi kuyasemea,” alisema Msekwa.
“Swali lako la msingi ni kama tunaweza kufikia hatua ya
kupinga matokeo ya urais na nimesema ndiyo tunaweza.”
Kada mkongwe wa CCM aliyewahi kuwa waziri katika utawala wa
Mwalimu Julius Nyerere na ambaye aliomba jina lake lisitajwe gazetini, alisema
hata kabla ya kupata Katiba mpya vyama vya upinzani vilishakubaliana na Kikwete
mambo manne, likiwemo la kupinga matokeo ya urais.
“Wagombea urais kupingwa mahakamani ni jambo zuri, “
alisema.
“Kimsingi vyama vya upinzani na na Rais Kikwete
walishakubaliana baada ya mchakato wa Katiba kukwama. Sijui kwa nini
hayakutekelezwa.
“Mambo manne waliyokubaliana ni kupinga matokeo ya urais,
mgombea urais atangazwe kushinda akifikisha asilimia 50 na zaidi ya kura, kuwa
na tume huru ya uchaguzi na kuwa na mgombea binafsi. walikubaliana kabisa,
sijui kwa nini hayakutekelezwa. Waulize wapinzani.”
Kwa upande wake Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, Dk Mohamed Bakari alisema ili Tanzania ifikie mabadiliko ya
Kenya, ni lazima mapambano ya kudai Katiba mpya yaongezeke.
“Ukichukua uzoefu wa Kenya, mpaka katiba imepatikana
kulikuwa na mapambano makali sana yakihusisha vyama vya siasa, asasi za kiraia
na wananchi wanaopenda demokrasia. Msukumo kama huo ni mdogo Tanzania,” alisema
Dk Bakari.
Kwa upande wake, Njelu Kasaka, waziri wa zamani enzi za
utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi, alisema ili kufikia mabadiliko ya Katiba ni
lazima wananchi wenyewe waidai.
“Nawapongeza Wakenya kwa sababu wameweza kujitawala kwa
kuweka uongozi wanaoutaka na kuuondoa wenyewe. Sisi tunaweza kufikia hatua hiyo
kwa kudai Katiba nzuri na kuweka taasisi zitakazoisimamia, kama Bunge na
Mahakama,” alisema Kasaka.
Alisema licha ya Tanzania kuwa mstari wa mbele katika vita ya
ukombozi wa Afrika miaka ya sitini, imebaki nyuma kidemokrasia tofauti na nchi
zilizokuwa nyuma.
“Tuliwalaumu makaburu wa Afrika Kusini kwa kukandamiza
demokrasia, tukasema demokrasia itawale hadi Zimbabwe, lakini leo tumeshindwa
kuwawajibisha viongozi wetu,” alisema.
“Wananchi waanze kudai Katiba mpya, lakini hatuwezi kuifikia
kama hatuna kambi ya upinzani imara. (Kama) Bado hatujawa na vyama vya upinzani
imara, kwa sababu kwa sasa vinabanwa na bado wananchi wengi hawaonyeshi mwamko.
Lazima tusawazishe nguvu ili kupata mabadiliko.”
No comments:
Post a Comment