KATAVI.
Mratibu wa uwezeshaji wananchi kiuchumi Mkoa wa Katavi Bw. Torokoko Kayumba amesema agizo la kuwa na viwanda vipya 100 kila mkoa katika kipindi cha mwaka mmoja linatekelezeka.
Ametoa kauli hiyo mapema leo wakati akizungumza na Mpanda Redio kwa njia ya simu na kusema wameanza kutekeleza agizo hilo na tayari wanaviwanda vipya viwili ambavyo vipo katika hatua ya awali.
Amefafanua kuwa kwa sasa serikali Mkoani Katavi imetenga maeneo katika kila halmashauri kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda huku akiwaomba wananchi kujitokeza katika kuanzisha viwanda.
Kwa mujibu wa Bw. Torokoko Mkoa wa katavi Kwa sasa una jumla ya viwanda vidogo 329, viwanda vya Kati 3 huku viwanda vikubwa kukiwa hakuna hata kimoja.
Kauli hiyo inakuja ikiwa leo ni siku ya uzinduzi kitaifa wa agizo hilo unaofanyika mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na mgeni rasimi ambaye ni waziri wa TAMISEMI Suleimani Jafo.
Source: Mdaki Hussein
No comments:
Post a Comment