Sunday, 19 November 2017

Jaji Mutungi atoa onyo kwa vyama vya siasa.



 Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amevionya vyama vya siasa na kutaka vifanye kampeni kwa kufuata sheria, vikijiepusha na vitendo vya matusi na uchochezi.
Kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata 43 zilizoanza Oktoba 26 zinaendelea na zitahitimishwa Novemba 25 na uchaguzi utafanyika Novemba 26.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Jumapili Novemba 19,2017 na Jaji Mutungi amesema maneno ya uongo, matusi na uchochezi kwenye kampeni ni kinyume cha sheria.
“Acheni kuchukua sheria mkononi na kutojihusisha na vitendo vya uchokozi, mfano kuingilia mikutano ya kampeni vya vyama vingine, kuchana na kuchoma moto bendera,” alisema.
Jaji Mutungi ameshauri vyama kujiepusha na propaganda zinazowatia hofu wapiga kura.
“Msijihusishe na vitendo vya rushwa kama vile kununua wapiga kura au kuuza shahada za mpiga kura,” amesema.
Amesema si vizuri kuziacha kasoro hizo ziendelee kuota mizizi na kwamba, ofisi yake itaendelea kuzikemea kwa nguvu zote.
Jaji Mutungi amesema vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi vina wajibu wa kisheria wa kuwaasa na kuwadhibiti wanachama na wagombea wao kufuata sheria.
Amesema maofisa wa ofisi hiyo wapo kwenye kata zote 43 wakifanya uangalizi ili kubaini ukiukwaji wa sheria.
“Wanaangalia ukiukwaji wa sheria ya vyama vya siasa na sheria ya gharama za uchaguzi,” amesema.
Msajili huyo amesema lengo ni kuhakikisha unakuwepo uwanja sawa wa ushindani katika uchaguzi, huku vyama vya siasa vikiwashawishi wananchi kwa sera zake na si vinginevyo.
Jaji Mutungi amesema miongoni mwa majukumu yanayotekelezwa na maofisa wake ni kutoa mafunzo elekezi kwa vyama vya siasa, wagombea wa udiwani, viongozi na wananchi kwa jumla.
Amesema mafunzo hayo yanahusu sheria ya gharama za uchaguzi na matendo yaliyokatazwa wakati wa kampeni.
“Naamini elimu hii itaendelea kuwaongezea wananchi ufahamu wa dhamira nzuri ya Serikali katika kukuza demokrasia nchini,” amesema
.

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...