Mjadala huu uliibua sababu mbalimbali za wasichana kukatisha masomo, zikiwamo umasikini wa wazazi ambao huwategemea mabinti kama vitega uchumi, kwa kupata mali ama kuwatuma wakatafute fedha walishe familia.
Sababu nyingine ni umbali kutoka shule hadi nyumbani. Hali hii huwafanya wasichana kupitia vishawishi lukuki wanapotoka ama kurejea nyumbani kutoka shule.
Hali hii inawafanya baadhi yao kuzidiwa na vishawishi vya wanaume na kujikuta wanaambulia ujauzito na mwishowe kutupwa nje ya mfumo wa elimu rasmi.
Ripoti nyingi ikiwamo ya takwimu za elimu inayotolewa kila mwaka na Serikali pamoja na ile ya waangalizi wa haki za binadamu (Human Rights Watch) ya mwaka 2016, zinaonyesha kuwa kati ya maelfu ya wanafunzi wanaoacha shule, wasichana ni waathirika zaidi ukilinganisha na wanafunzi wa kiume
Kwa mfano, takwimu za Serikali mwaka 2016, zinaonyesha wanafunzi 3,439 waliacha na kukatishwa ndoto zao baada ya kupata mimba.
Kwa upande wake, ripoti ya waangalizi wa haki za binadamu mwaka huohuo ilionyesha kuwa takribani wasichana 8,000 huacha shule kila mwaka, kutokana na kukatishwa masomo baada ya kuolewa ama kupata mimba wakiwa wadogo.
Idadi hiyo ni kwa wale wanaofikiwa na tafiti ama kujulikana, lakini wapo wasichana ambao baada tu ya kupata ujauzito, hufichwa na taarifa zao kutowekwa wazi shuleni wala katika jamii, kwa sababu ya wazazi huhofia kukutwa na mkono wa sheria.
Mjadala bungeni
Katikati ya mjadala huu, wapo baadhi ya wadau ambao walipaza sauti zao wakitaka kuangalia namna ya kuwarejesha shule wasichana, ambao kwa bahati mbaya walipata mimba wakiwa masomoni. Suala hili limeibua mjadala mzito ambao haujapatiwa majibu ya kina.
Baadhi ya wabunge wakiwa bungeni mjini Dodoma, waliunga mkono umuhimu wa kuwarejesha shule wasichana wanaojifungua, ili kuwafanya watimize ndoto zao baada ya kujifungua na kuondoka kwenye mduara wa umasikini.
Hata hivyo, hawakugusia namna ya kumaliza vikwazo vingine vinavyowarudisha nyuma wasichana kuendelea na masomo.
Kwa upande mwingine, hoja ya kuwarejesha shule wasichana wazazi ilipingwa na baadhi ya wabunge, waliosema kufanya hivyo ni sawa na kuruhusu ngono holela kwa wanafunzi na kuhalalisha utovu wa nidhamu kwa kuwaruhusu ‘wazinzi’ kuendelea na masomo.
Tujiulize
Yumkini suala ambalo inatupasa kujiuliza ni je, wasichana wanaorubuniwa na walimu, wazazi ama walezi ama wanaobakwa na kujikuta wana ujauzito, wanasaidiwa vipi ilihali walipata mimba bila ridhaa yao?
Uchunguzi uliofanyika Agosti mwaka 2017 katika wilaya 11 kwa uratibu wa HakiElimu, ulibainisha sababu nyingi zinazochangia mimba za utotoni, zikiwamo mmomonyoko wa maadili, umbali wanaokabiliana nao wanafunzi kwenda na kurudi shule.
Nyingine ni umasikini, ukosefu wa mabweni, malezi mabovu ya walezi na wazazi na utandawazi.
Katika machimbo ya madini ya Lwamgasa, mkoani Geita, baadhi ya wasichana wanalazimika kutembea umbali mrefu kufuata shule huku wengine wakilazimika kupanga vyumba maarufu kama ‘geto’, huku kila siku wakikutana na vijana ambao huwarubuni kwa kiasi kidogo cha fedha au kwa lifti za bodaboda na baadaye kuwaomba ngono.
Baadhi ya wasichana wanakiri kukabiliana na vishawishi vingi kutoka kwa wanaume, huku baadhi wakiripotiwa kupotea na wanaume na baadaye kuonekana. Wengine huwa hawarejei shule kabisa.
Wapo wasichana ambao huwindwa na wenye nyumba wanazopanga, hali ambayo hata wasipopata mimba, usumbufu wanaoupata huwafanya wakose utulivu na uzingativu wa masomo.
Wapo wanaotamani tu kuwa na wasichana wadogo kwa sababu za kuzichoka ndoa zao. Wengine wanatamani kuwa na wanafunzi kwa sababu wanaamini ni kundi rahisi na halina gharama za kuwatunza tofauti na wanawake watu wazima wenye mahitaji lukuki.
Katika wilaya ya Kilombero kwa mfano, walanguzi wa mchele huwarubuni wasichana.
Kwa mujibu wa ofisa maendeleo wa halmashauri hiyo, Latifa Kalikawe, jamii ya eneo hilo ina utaratibu wa kuwaachia wasichana jukumu la kulea familia, hivyo kuwaweka mabinti katika hatari ya kurubuniwa kwa ‘misaada’ ya walanguzi hao, ili kuokoa familia zao kwa fadhila mbalimbali ikiwamo ngono.
Tuwasaidie watoto wa kike
Kwa kuzingatia hali hiyo inatupasa kumsaidia binti aweze kutimiza ndoto zake, kwa kuacha kuwarubuni watoto wa kike kimapenzi.
Aidha, wazazi wanapaswa watimize wajibu wao wa kuwafundisha wasichana kujiheshimu na kamwe kutoruhusu mtu yeyote kuwagusa kabla ya kufikia umri unaoruhusiwa kuwa na uhusiano na kuolewa.
Lengo kuu la kampeni ya Ondoa Vikwazo Asome, lilikuwa ni matarajio kwamba jamii itaamka na kuchukua hatua za kuondoa vikwazo kwa watoto wa kike.
Hatua hizo zingelenga kumlinda mtoto wa kike kwa kuwajengea mabweni, kuwakinga na vitendo vya unyanyasaji, kutoruhusu wasichana kuolewa katika umri mdogo. Kikubwa zaidi ni kuhakikisha kila mwanajamii anakuwa mlinzi wa mtoto wa kike.
Nchi ya Uganda inatajwa kama mfano ambapo ni nadra kwa mwanaume kuonekana akimrubuni msichana na jamii ikakaa kimya.
Kama Taifa tuendelee kutafakari nini kifanyike kwa wasichana ambao wameachwa na mfumo rasmi wa elimu.
Chanzo:Mwananchi
#Changia Damu Okoa Taifa
No comments:
Post a Comment