Makundi ya wanawake kutoka mashirika tofuati nchini Kenya yameandamana hii leo ya kuishinikiza serikali kuchukua hatua kuhusiana na madai kuwa akina mama waliojifungua wamekuwa wakidhulumiwa kingono katika Hospitali kuu ya Taifa, Kenyatta National Hospital.
Maandamano hayo yanafanyika wakati ambapo ripoti ya uchunguzi uliyoagizwa na waziri wa afya nchini humo inatarajiwa kutolewa rasmi.
Waziri wa afya nchini Kenya Dkt Cleopha Mailu aliagiza uchunguzi kufanywa katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta baada ya wanawake waliojifungua kudai kwamba wanadhalilishwa kingono.
Taarifa zilizoenezwa kwenye mitandao siku ya Ijumaa zinadai kina mama waliojifungua wamekuwa wanashambuliwa na baadhi ya wafanyikazi wakati wakienda kwenye chumba cha watoto wachanga kuwanyonyesha watoto wao.
Wanaotuhumiwa ni wahudumu katika vyumba vya maiti, wanaonyooshewa kidole pia kwa kutumia maiti kuwashutua akina mama waliojifungua katika hospitali hiyo.
Wanaharakati wa kutetea haki za wanawake wanaoandamana leo katika mji mkuu, wanasema dhamira yao kuu kumiminika barabarani ni kutaka mabadiliko yafanyike, na kwamba usalama wa wanawake ni jambo linalopaswa kutiliwa umuhimu.
Mildred Atty ni mojawapo ya waandalizi wa maandamano hayo.
Katika mahojiano amesema, 'limekuwa likiendelea kwa muda usiojulikana, na ni lazima liishe'.
Hospitali ya taifa ya Kenyatta, Nairobi huwahudumia kina mama takriban 100 wanaojifungua kila siku.
Maswali sasa yameanza kuulizwa kuhusu muundo na mpangilio wa vyumba katika hospitali hiyo ambao huwalazimu kina mama waliojifungua kupanda ngazi au lifti kwenda kuwanyonyesha watoto wao, ikizingatiwa kwamba baadhi hujifungua kupitia upasuaji.Watoto waliozaliwa huwekwa chumbani ghorofa ya kwanza nao wanawake kwenye wodi za kujifungulia kwenye ghorofa ya chini.
Maswali sasa yameanza kuulizwa kuhusu muundo na mpangilio wa vyumba katika hospitali hiyo ambao huwalazimu kina mama waliojifungua kupanda ngazi au lifti kwenda kuwanyonyesha watoto wao, ikizingatiwa kwamba baadhi hujifungua kupitia upasuaji.
Chanzo:Bbc swahili
#Changia Damu Okoa Taifa
No comments:
Post a Comment