Friday, 2 February 2018

Magufuli akerwa na dosari za Mahakama


Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli

RAIS John Magufuli ametoa wito kwa Idara ya Mahakama, kuendelea kurekebisha dosari, ambazo zimekuwa zikiuchafua mhimili huo wa Dola. Baadhi ya dosari hizo ni majaji na mahakimu kujihusisha na vitendo vya upokeaji wa rushwa na ucheleweshaji wa kesi, ambavyo vinasababisha hasara kubwa kwa Taifa.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika jijini Dar es Salaam jana, Rais Magufuli alimtaka Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma, kushughulikia dosari hizo haraka ili kurejesha imani ya wananchi kwa chombo hicho muhimu. “Mwaka jana nililalamika, sasa mwaka huu sitalalamika, nitachukua hatua, tena mwezi huu wa pili hautaisha, pale ofisini kwangu napokea barua nyingi za malalamiko ya ucheleweshaji wa kesi, kila kesi upelelezi haujakamilika, ni lazima kuwe na utatuzi wa jambo hili, alisema Rais Magufuli.
Katika kuonesha namna hatua hiyo inavyolitia hasara Taifa, Rais Magufuli alisema hivi sasa kuna kesi za Sh bilioni 169.1 na Dola za Marekani milioni 38.2 zinasubiri tu bila kutolewa maamuzi na hivyo nchi inakosa mapato. Kesi hizo zipo katika Baraza la Kodi na Baraza la Usuluhishi. Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alimpongeza Jaji Mkuu kwa hatua alizochukuwa kuwafukuza kazi watumishi 112 wa Mahakama, wakiwemo Mahakimu 17 waliojihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili.
Alivishangaa vyombo vingine ambavyo hushirikiana na Mahakama kama vile Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Magereza na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwa kutowawajibisha watumishi wake, wanaokiuka maadili.
Alisema japokuwa Sekta ya Mahakama imefanya kazi nzuri katika kutoa haki katika miaka ya hivi karibuni, bado utafiti wa Taasisi ya Twaweza uliotolewa hivi karibuni umeitaja Idara ya Mahakama na Polisi kuwa ndizo zinaongoza kwa vitendo vya rushwa. Aliagiza ufanyike uchunguzi dhidi ya majaji wengi, walioomba kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya likizo wakiambatana na familia zao, huku wakikaa kwenye hoteli za kifahari kwa siku zaidi ya 28 na kujigharamia wenyewe wakati mishahara yao ni ya kawaida. “Ndiyo maana nasema utafiti huu si wa kupuuzwa lazima ufanyiwe kazi.
Mimi mwenyewe nimetoa vibali vingi vinavyoombwa na Majaji wakiomba ruhusa ya kwenda likizo nje ya nchi, mara Afrika Kusini, Dubai na sehemu nyingine. “Majaji hawa wanakwenda na familia zao wanakaa kwa siku 28 na zaidi na wanaandika wazi kabisa watajigharamia wenyewe wala hawaombi fedha serikalini. “Nimewafuatilia wanapokaa kwenye mahoteli makubwa, wanakula, kulala na kunywa mpaka sasa sipati majibu wamepata wapi fedha za kujigharamia hivyo, wakati mishahara yao inajulikana,” alisema Rais Magufuli.
Alimtaka Profesa Juma kutumia Tume ya Utumishi wa Mahakama, kutathmini na kuchunguza safari hizo kwani vitendo vya aina hiyo, ndiyo vinavyoichafua sekta hiyo ya Mahakama na kuonekana ya watu wasio waadilifu. Pamoja na hayo, Rais Magufuli alikiri kuwa pamoja na kuwepo kwa tatizo la uadilifu, bado ucheleweshwaji wa kesi ni tatizo.
Alisema kwa sasa kuna changamoto ya mlundikano wa kesi katika Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani huku idadi ya Majaji ikiwa haitoshelezi, jambo ambalo hata hivyo, alibainisha linasababishwa na baadhi ya watendaji wa vyombo vinavyotoa haki kutotimiza wajibu wao. Alisema anazo taarifa za kuwepo kwa kesi, ambazo tayari zimekamilika na zinahitaji kutolewa hukumu, lakini baadhi ya watendaji wa vyombo vinavyotoa haki wamekuwa wakitoa sababu zisizo za msingi na kuchelewesha haki kupatikana.
“Utakuta kuna kesi ya mtu kakamatwa na dawa za kulevya au meno ya tembo, ushahidi na kila kitu kipo, lakini inapofika mahakamani, mpelelezi anasema uchunguzi unaendelea. Matokeo yake baada ya muda ule unga wa dawa za kulevya unasikia si dawa za kulevyabali ni unga wa udaga, haya ndiyo mazingira ya kujitengenezea rushwa,” alisisitiza.
Alisema kutokana na ucheleweshwaji wa kesi, zipo athari nyingi ikiwemo kusababisha migogoro katika jamii na kusababisha athari za kiuchumi, ambapo kwa sasa yapo mashauri 139 yanayohusu kodi yaliyofunguliwa kwenye Baraza la Kodi na Baraza la Usuluhishi za kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka 2015. Alisema kuchelewa kutolewa maamuzi kwa mashauri hayo yenye thamani ya Sh bilioni 169.1 na dola za Marekani milioni 38.2, kunaisababishia ukosefu wa fedha serikali endapo kutakuwa na mashauri ambayo serikali itashinda.
“Hata hivyo kuna usemi kuwa unapochelewesha haki ni sawa na kumnyima mtu haki yake. Naziomba mamlaka husika zichukue hatua kudhibiti tatizo hili la ucheleweshwaji wa kesi na kama kuna watu wanazichelewesha kwa maslahi yao wachukuliwe hatua,” elieleza. Aliipongeza sekta ya Mahakama kupitia Tume ya Utumishi wa Mahakama, kwa hatua ilizochukua dhidi ya watendaji wasio waadilifu 112, ambao kati yao 27 walikuwa ni Mahakimu waliostaafishwa kwa lazima na wengine kustaafishwa kwa tuhuma mbalimbali za ukosefu wa maadili.
Alisema japokuwa Mahakimu wengi waliopandishwa kizimbani walishinda kesi, lakini Jaji Juma alichukua uamuzi wa kuwastaafisha kwa lazima kutokana na ukweli kuwa hakimu akishapandishwa kizimbani kwa rushwa haipendezi. “Halafu pia kesi hizi zilikuwa zinasikilizwa na mahakimu, pia ni sawa na kesi ya nyani umpelekee ngedere,” alisema Rais Magufuli.
Hata hivyo, alisema pia kulikuwa na Mahakimu 14 waliofukuzwa kazi na watumishi 64 kutokana na ukosefu wa maadili. “Natoa wito kwa vyombo vingine vinavyosimamia utolewaji wa haki kama vile Polisi, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) na Magereza kuiga mfano wa Sekta hii ya Mahakama na kuwachukulia hatua wale wote wanakwenda kinyume na maadili na kujihusisha na rushwa.
“Leo hii nilitegemea Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Mkuu wa Magereza na Takukuru mngeniletea orodha ya watu wenu mliowafukuza kwa makosa mbalimbali ikiwemo kuwabambikia watu kesi, kuchelewesha kesi na kula rushwa, kuingiza simu magerezani au dawa za kulevya,” alisema. Pamoja na hayo, Rais Magufuli alioneshwa kusikitishwa na utendaji wa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu (DPP), kutokana na kesi nyingi za serikali kushindwa Mahakamani, huku wanasheria wazuri wakihamishwa na wengine kupelekwa Ikulu.
“Hali hii haipendezi ndiyo maana serikali tunashindwa kesi nyingi tu. Naomba Majaji mtuvumilie tu, hili suala nitalishughulikia na najua tatizo lililopo, huu mwezi wa pili hauishi,” alisisitiza. Akizungumzia kaulimbiu ya siku hiyo ya Mahakama inayosema matumizi ya ‘Tehama katika Utoaji Haki Kwa Wakati na Kwa Kuzingatia Maadili’, alisema imekuja kwa wakati kwani matumizi ya Tehama, yatatoa fursa nzuri ya kushughulikia mfumo wa Mahakama.
Alisema Tehama itapunguza mlundikano wa kesi, kwa kuwa sasa kesi zitaweza kusikilizwa hata kwa njia ya video za moja kwa moja, kudhibiti uzembe wa upotevu wa mafaili au kutokujua kesi fulani iko wapi au kwa jaji gani, na kudhibiti uvunjifu wa maadili kama vile rushwa na urasimu.
Kuhusu rushwa, Rais huyo aliwataka Watanzania watambue kuwa mihimili yote mitatu, Bunge, Serikali na Mahakama, haiongozwi na malaika bali binadamu na kwamba anazo taarifa kuwa wapo majaji, wabunge na hata mawaziri wanajihusisha na rushwa. “Nina information nyingi tu, nimeamua kuzungumza hapa hadharani kwa sababu nataka tijirekebishe, tusonge mbele najua pia wapo watu wanaojihusisha na dawa za kulevya kwa hiyo jamani badilikeni,” alisema.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu Profesa Juma alisema Mahakama nchini imepiga hatua katika kutoa huduma zake ikiwemo kupunguza mlundikano wa kesi, ambapo kwa upande wa Mahakama za mwanzo, wilaya na hakimu mkazi, idadi ya mashauri yaliyolundikana imepungua, ambapo kwa sasa Mahakama ya Mwanzo ni asilimia sifuri.
Alisema katika Mahakama za Wilaya na Hakimu Mkazi, idadi ya mashauri 2,334 ndiyo yaliyozidi umri wa miezi 12 na kuingia kwenye kundi la mlundikano, sawa na asilimia tisa ya mashauri 25,658 yaliyopo. Hata hivyo, alieleza kuwa changamoto kubwa ipo kwenye Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani, ambako kuna mlundikano wa kesi huku idadi ya majaji ikiwa haijitoshelezi.
Alisema katika Mahakama Kuu takwimu zinaonesha kuwa kuna jumla ya mashauri 16,487 yaliyofunguliwa pamoja na mashauri 16,703 yaliyobaki, hivyo kufanya Mahakama hiyo kuwa na mashauri 33,190 kwa kipindi cha Januari ukilinganisha na mashauri 28,307 ya mwaka 2012, 30,182 ya mwaka 2013, 35,050 ya mwaka 2014, 31,521 ya mwaka 2015, 36,562 ya mwaka 2016 na 33,190 ya mwaka jana.
“Ongezeko hili ni kubwa limezidi wastani wa uwezo wa jaji kufanya kazi yake kwa ufanisi. Takwimu zinaonesha idadi ya majaji wa Mahakama Kuu imepungua kutoka majaji 64 mwaka 2012, 59 mwaka 2013, 71 mwaka 2014, 84 mwaka 2015, 75 mwaka 2016 na 62 mwaka jana,” alieleza.
Alisema idadi ya majaji kuendelea kupungua na mashauri kuongezeka, kunafanya wastani wa mashauri kwa kila Jaji kwa miaka sita mfululizo kuwa mzigo, ambapo mwaka 2012 Jaji mmoja alikuwa na mashauri 442, mwaka 2013 mashauri 512, mwaka 2014 mashauri 494, mwaka 2015 mashauri 375, mwaka 2016 mashauri 487 na mwaka jana mashauri 535.
Kwa upande wa Mahakama ya Rufaa, alisema idadi ya Majaji imeendelea kuwa 15 bila mabadiliko kwa miaka hiyo sita, lakini idadi ya mashauri imeongezeka ambapo mwaka 2012 kulikuwa na mashauri 2,466, mwaka 2013 mashauri 2,629, mwaka 2014 mashauri 2,916, mwaka 2015 mashauri 3,244, mwaka 2016 mashauri 3,975 na mwaka jana mashauri 4,439.
Aidha, alisema katika kudhibiti uvunjifu wa maadili, Tume ya Utumishi wa Mahakama ilipokea malalamiko ya watumishi 143, kati yao waliofukuzwa au kuondolewa na kustaafishwa ni 112, watumishi 17 uchunguzi unaendelea na 14 wamepewa onyo. Akielezea kaulimbiu ya Mahakama kuanza kutumia Tehama katika utendaji wake alisema sekta hiyo haitaki kubaki nyuma na kubaki na aibu ya nyaraka na majalada kupotea na wateja kutofahamu mahali kesi zao zilipo.
Chanzo:Habari leo
#Changia Damu Okoa Taifa

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...