SONGWE
Mkoa wa Songwe na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini Nchini
(TARURA) wameingia makubaliano kwa kuwekeana saini mikataba tisa ya barabara,
madaraja 10 na kalavati 18 vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh1bilioni.
Akizungumza baada ya kuwekeana saini mikataba hiyo, mjini
Vwawa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku
Galawa ameitaka Tarura na wakandarasi kutengeneza barabara za vijijini kwa
viwango na ubora sawa na mjini.
Pia amewataka waache fikra za kutofautisha barabara za vijijini
na mijini badala yake wazingatie kuongeza uchumi wa wakazi wa maeneo hayo
kwa kuwaboreshea miundombinu ya barabara.
Galawa ametaka kuwepo na njia maalumu ya kupitisha mifugo badala
ya kuiacha ikipita barabarani na kuziharibu, pia kuwaondoa mapema wote
wanaofanya shughuli za kibinadamu katika eneo la hifadhi za barabara.
Mratibu wa Tarura mkoani Songwe, Mhandisi Ernest Mgeni amesema
mchakato wa kuwapata makandarasi walioshinda zabuni hiyo ulianza Novemba 13
mwaka jana kwa kutangaza zabuni nchi nzima zenye kazi 21 za matengenezo ya
barabara na kuwapata washindani 104.
Chanzo:Mwananchi
#Changia Damu Okoa Taifa
No comments:
Post a Comment