Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimedai kuwa kipo tayari kumuongoza Rais John Magufuli katika kulinda rasilimali za Taifa ikiwemo madini, huku kikiwataka wananchi kuishauri serikali kuchukua hatua kwanza badala ya kuipongeza kuhusu sakata la Makinikia.
Chadema imesema iwapo Tanzania inataka kunufaika na rasilimali zake na kushinda vita vya kutetea utajiri wake inapaswa kwanza kurejesha katiba iliyopendekezwa na Jaji Joseph Warioba na si vinginevyo.
Akitoa msimamo wa chama kutokana na kile kinachoendelea baada ya kutolewa kwa ripoti mbili za Rais kuhusu mchanga wa dhahabu, leo (Ijumaa) Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vincent Mashinji amesema suluhisho la kudumu katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za Taifa ni kurejea katika katiba ya wananchi.
Katibu Mkuu Chadema, Dkt. Vincent Mashinji amedai kuwa, hatua anazochukua Rais Magufuli kuhusu Makinikia ziko kinyume na Ilani ya CCM ambapo katika ukurasa wake wa 26-28 haikuzungumzia kurekebisha sheria na mikataba ya madini, na kwamba ilani ya Chadema kwenye ukurasa wake wa 57-59 inaonyesha namna ya kuiongoza vizuri sekta ya madini.
“Rais hatafaulu vita hii kama serikali yake itaendelea kutubagua au kutosikiliza sauti ya upande wa pili. Pia watu wasiwe wa kutoa pongezi kabla kazi haijaisha. Kama tunatakiwa kulipwa trilioni mia, wajue kwamba za kwetu ni asilimia 4 tu, na hii ndiyo matokeo ya mikataba tuliyoilaani kila siku. mrabaha wetu ni asilimia 4 huku wawekezaji kwenye pesa hizo za kwao ni 96%,” amesema.
“Chadema tunasema kuwa haya yote tunayoyapigia kelele itakuwa ni kazi bure iwapo haturejeshi hoja ya katiba mpya.
“Katiba ya Warioba iliweka mapendekezo ya jinsi ya kulinda rasilimali za taifa na kama tungefuata hayo yote hili la sasa halingepaswa kuwa na mjadala mkubwa kiasi hiki,” amesema wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya chama hicho Kinondoni.
No comments:
Post a Comment