Monday, 28 August 2017

JPM aombwa aingilie kati mgogoro wa ardhi Chanika.


Rais wa Tanzania Dk. Jonh Mgufuli
Wakazi wa Chanika wilayani Ilala wamemuomba Rais John Magufuli angilie kati mgogoro wa ardhi ikiwamo kufanyiwa uhakiki wa mipaka kati ya msitu wa hifadhi wa Kazimzumbwi na wananchi wanaoishi jirani na eneo hilo.
Mgogoro huo wa ardhi kati ya wakazi wa Nzasa, Nyeburu, Kimwani na hifadhi hiyo umedumu kwa miaka 19.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema mgogoro huo ulianza mwaka 1998 na kwamba Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) ilitoa notisi ya siku mbili na nyumba zaidi ya 200 zilibomolewa.
Mkazi wa Nyeburu, Limboa Limboa alisema mwaka 2012 iliundwa kamati ya wakulima wa maeneo hayo kufuatilia ndipo Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wa wakati huo, Profesa Anna Tibainyuka alitoa tamko bungeni akisema wananchi hao wapo nje ya msitu huo hivyo waendelee na shughuli zao.
Alisema cha kushangaza mwaka 2014 maliasili walikwenda kwenye maeneo yao na kuvunja nyumba zaidi ya 200 wakidai wapo kwenye eneo la hifadhi hiyo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Habedi Chande alisema baada ya tukio hilo kutokea waliandika barua mbalimbali ndipo Julai 30 mwaka huu walionana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na kuwaeleza kuwa alituma wataalamu wake na vielelezo vyote amekabidhiwa waziri mkuu.
“Cha kushangaza hawa maliasili wanasema wanatuhamisha eneo hili wakidai wametushinda kesi tuliyofungua Mahakama Kuu ya Ardhi, hivyo hatujawahi kufungua kesi sehemu yeyote ile huu ni mpango wa wapiga dili kutaka kutudhulumu ardhi yetu,” alisema Chande.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Nyeburu, Hamisi Geo alimuomba Rais Magufuli atakapofanya ziara eneo la Chanika ashughulikie tatizo hilo kwa madai kuwa maliasili wamekuwa wakiwanyanyasa wakazi wanaoishi karibu na eneo hilo.
Msemaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Doreen Makaya aliwataka wakazi hao kwenda kwenye ofisi hiyo ili wasikilizwe kilio chao na si kulalamika kwenye majukwaa.

“Huo mgogoro ni wa muda mrefu kati ya wananchi hao na msitu wa hifadhi ya Kazimzumbwi kinachotakiwa waje ofisini ili wasikilizwe,” alisema Makaya.

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...