Rais wa
Marekani, Donald Trump, ametetea matamshi yake ya baada ya ghasia za
Charlottesville na kuvilaani vyombo vya habari kwa kutokuwa na uaminifu, katika
mkutano huko Arizona. Maelfu ya raia pia waliandama kumpinga.
Trump alikabiliwa na kauli
za hasira baada ya kusema kwamba anazilaumu 'pande nyingi' kwa ghasia
zilizotokea Charllotesville Virginia, zilizosababisha kifo cha mwandamanaji
aliyekuwa akipinga ufashisti.
Akirudia tena matamshi yake
aliyoyatoa kufuatia ghasia hizo za Charlottesville, Trump akiwa mjini Phoenix,
Arizona, alivilaumu vyombo vya habari kwa kumtafsiri vibaya.
" Watu pekee wanaotoa
jukwaa kwa vikundi hivi vya chuki ni vyombo vya habari, pamoja na habari za
uongo," amesema Donald Trump.
Hotuba hiyo ilikuja
mwishoni mwa ziara ya Trump katika jimbo la Arizona, ambayo ikulu ya Marekani -
White House- ilitarajia kuwa itawashawishi zaidi wafuasu wa Trump na kuongeza
kasi juu ya mpango wenye utata wa kujenga ukuta katika mpaka kati ya Marekani
na Mexico.
Pia kulikuwa na wafuasi wa
Trump, waliokuwa wakipiga mayowe ya kutaka kujengwa kwa ukuta huo. Wengi
walivalia kofia nyekundu yenye kauli mbiu ya kampeni ya Trump ya wakati wa
uchaguzi uliopita, inayosema "jenga tena Marekani iliyo bora”
Rais wa Marekani pia
aligusia juu ya uwezekano wa kumsamehe Joe Arpaio, mkuu wa polisi wa zamani
aliyehukumiwa mwezi uliopita katika kesi inayohusu makosa ya ubaguzi wa rangi.
Arpaio, aliyekuwa mkuu wa
polisi wa kaunti ya Maricopa huko Phoenix kabla ya kushindwa katika uchaguzi
mpya mwaka 2016. Ni mpinzani mkubwa wa uhamiaji kinyume cha sheria. Arpaio
mwenye umri wa miaka 85 pia alijulikana kwa kuchunguza hati ya kuzaliwa ya rais
wa zamani wa Marekani, Barack Obama, na kudai bila ya ushahidi wa msingi kwamba
hati hiyo ilikuwa ya uwongo.
Trump alianza siku yake
katika mji Yuma kwa kutembelea kituo cha operesheni za doria za mpakani
alikozungumza na walinzi wa mpakani. Baada ya hapo Trump alielekea mji wa
Phoenix kwa mkutano uliofanana na wa kampeni ambapo alitambulishwa kwa umati wa
watu Makamu wa Rais Mike Pence.
Trump pia aligusia masuala
mengine kadhaa ikiwa ni pamoja na makubaliano ya biashara ya mataifa ya Amerika
Kaskazini (NAFTA), mvutano kati ya Marekani na Korea Kaskazini na mambo mengine
kadhaa katika hotuba hiyo iliyochukuwa takriban saa moja na dakika 15.
Wakati hayo yakijiri,
maelfu ya watu waliandama nje ya eneo alipokuwa akihutubia Trump kumpinga rais
wao. Polisi waliwatawanya kwa kutumia kemikali ya kuwasha baada ya kurushiwa
mawe na chupa na waandamanaji hao.
Idadi kamili ya watu
waliojitokeza katika maandamano hayo haikuwekwa wazi na maafisa wa polisi
lakini vyombo vya habari vya Arizona vimesema vimekadiria watu hao walikuwa kwa
maelfu.
Watu
wanne walitiwa mbaroni na polisi wakati wa maandamano hayo, watatu kati yao kwa
madai ya kufanya mashambulizi, amesema mkuu wa polisi ya Phoenix, Jeri
Williams, wakati wa mkutano na waandishi habari.
No comments:
Post a Comment