Tuesday, 12 September 2017

Uchunguzi waanza Mwadui Sakata la madini lapeleka msururu wa vigogo Takukuru.

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru,Valentino Mlowola

 Dar es Salaam. Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) inawahoji vigogo wa Serikali wakiwamo waliokuwa mawaziri wa Nishati na Madini kwa nyakati tofauti huku polisi ikitua katika mgodi wa almasi uliopo Mwadui.
Taarifa ambazo gazeti hili limezipata zilisema miongoni mwa vigogo waliohojiwa na Takukuru kwa vipindi tofauti mpaka jana ni mawaziri wa zamani wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na William Ngeleja.
Akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili jana, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola japo hakuwataja mawaziri hao wastaafu alikiri vigogo kadhaa kuhojiwa.
Mwandishi: Kuna taarifa kuwa Takukuru inawahoji waliokuwa mawaziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na William Ngeleja. Ni kweli?
Mlowola: Wanaohojiwa hapa ni wengi.
Mwandishi: Sawa, lakini nilitaka kujua kama kweli hao wawili leo mnawahoji?
Mlowola: Unajua tumekabidhiwa jukumu la kuchunguza masuala ya madini, kwa hiyo hilo linafanyika hapa.
Mbali ya ripoti za kamati teule za Bunge zilizochunguza mwenendo wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa madini ya almasi na Tanzanite zilizowasilishwa kwa Rais John Magufuli kuwataja Profesa Muhongo na Ngeleja, pia ziliwataja aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene na Naibu Waziri wa Ujenzi, Edwin Ngonyani kuhusika kwa namna moja au nyingine katika masuala ya kiutendaji yaliyokwenda kinyume na mikataba.
Hata hivyo, Rais Magufuli alisema Profesa Abdulkadir Mruma aliyetajwa katika ripoti hiyo kuwa mmoja wa wahusika alikuwa alipandikizwa kwa maadui ili kuibua taarifa ya namna nchi inavyoibiwa.
Profesa Mruma ndiye aliyeongoza kamati ya kwanza ya Rais ya kuchunguza mchanga wa madini ambayo pamoja na mambo mengine ilimtaja Profesa Muhongo kuhusika na upotevu wa mapato ya madini na hivyo kutakiwa kujiuzulu Mei 24.
Ngeleja ambaye pia alikuwa Waziri wa Nishati na Madini katika awamu ya nne ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete alitajwa katika kashfa kadhaa za madini ikiwamo ya mchanga wenye madini maarufu kama makinikia.
Mbali na kashfa hiyo, vilevile alitajwa katika kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow ambayo hata hivyo hivi karibuni alitangaza kurejesha Sh40 milioni zilizotolewa na mfanyabiashara James Rugemalira.
Mawaziri wengine wastaafu wa Nishati na Madini katika awamu ya tatu na nne waliotajwa katika kashfa za madini na kamati za Rais ikiwamo ile ya pili ya makiniki iliyoongozwa na Profesa Nehemia Osoro ni pamoja na Daniel Yona, Abdallah Kigoda (marehemu) na Nazir Karamagi.
Wengine waliotajwa ni waliokuwa wanasheria wakuu wa Serikali; Andrew Chenge na Johnson Mwanyika.
Vilevile wamo aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Mikataba, Felix Mrema na waliokuwa makamishna wa Wizara ya Nishati na Madini, Mary Ndosi na Dk Dalali Kafumu, wanasheria akiwamo Jaji Julius Malaba na baadhi ya maofisa wa TRA.
Akizungumza baada ya kupokea ripoti za biashara ya almasi na Tanzanite wiki iliyopita, Rais Magufuli aliagiza viongozi wote waliotajwa katika ripoti hiyo kujiuzulu mara moja kupisha uchunguzi.
Pia, aliagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuwakamata wote waliotajwa, huku akiwataka Watanzania kuwa na uzalendo.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro alisema jeshi hilo limeshaanza kufanyia kazi ripoti walizokabidhiwa na Rais Magufuli kuhusu masuala ya wizi, ufisadi, uzembe pamoja na rushwa zilizosababisha nchi kupata hasara kutokana na biashara ya madini.
“Wale wote waliotajwa kwenye ule uchunguzi wa biashara ya madini ni vizuri sana wakajisalimisha wao wenyewe kwa mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai ili waweze kuhojiwa na uchunguzi ufanyike halafu tuweze kufahamu wanahusika kwa kiasi gani na wasisubiri kukamatwa,” alisema.
Maofisa Tanzanie One washikiliwa
Maofisa saba wa kampuni ya Tanzanite One inayochimba madini ya Tanzanite katika eneo la Mererani wilayani Simanjiro wakiwamo wakurugenzi wawili wanashikiliwa na polisi mkoani Manyara kwa mahojiano kutokana na taarifa za utoroshwaji wa madini ya Tanzanite.
Wakati maofisa hao wakishikiliwa Jeshi la Polisi mkoani humo hivi sasa limechukua jukumu la ulinzi wa migodi ya Tanzanite iliyopo sehemu hiyo ili kuzuia vitendo vyovyote vya utoroshaji wa madini na uvamizi ndani ya Tanzanite One.
Akizungumza na Mwananchi jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Francis Massawe alisema maofisa hao wanahojiwa kutokana na tuhuma za utoroshwaji wa madini kama ambavyo iliainisha na kamati ya Bunge iliyoundwa kuchunguza sekta ya Tanzanite.
Massawe alisema wakurugenzi wa Tanzanite One ambao wanashikiliwa ni Hussein Gonga na Faisal Shabhai na pia kuna maofisa wengine watano ambao wanaendelea kuhojiwa.
“Tumewashikilia kupata taarifa kuhusiana na tuhuma mbalimbali ambazo zimetolewa na kamati ya Bunge,” alisema.
Akizungumzia ulinzi katika migodi ya Tanzanite, Massawe alisema jeshi hilo limeongeza askari wake ambao watalinda migodini ili kuzuia utoroshaji wa madini. “Kuanzia sasa tutakuwa tunalinda migodini ili kulinda watu wasitoroshe madini na kuhakikisha tunadhibiti matukio ya uvamizi migodini,” alisema
Kukamatwa kwa maofisa hao kumetokana na agizo la Rais Magufuli linalotaka ufanyike uchunguzi juu ya tuhuma mbalimbali huku pia viongozi wa Serikali waliotajwa wakitakiwa kujiuzulu kupisha uchunguzi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Nishati na Madini, Kampuni ya Tanzanite One inamilikiwa kwa ubia baina ya Shirika la Madini ya Taifa (Stamico) na kampuni ya Sky Associates Group Limited kuanzia Januari 30 mwaka 2015 .
Kampuni hiyo inamilikiwa na Hussein Gonga mwenye hisa 35, Faisal Shabhai hisa 25 na Rizwan Ullah mwenye hisa 40.
Katika mgodi huohuo wenye leseni ya ML 490/2013 uliopo eneo la kitalu C, Stamico kwa sasa inamiliki asilimia 50 ya hisa na Sky Associates asilimia 50 ya hisa.
Akizungumzia kamatakamata ambayo inaendelea Mererani, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Manyara, Sadiki Mnenei aliwataka wanachama wao kuwa watulivu wakisubiri uchunguzi wa Serikali.
“Ni kweli kuna wachimbaji wanashikiliwa kwa ajili ya uchunguzi, sisi kama chama tunawataka wachimbaji kuwa watulivu kipindi hiki,” alisema.
Kutoka Shinyanga, kikosi maalumu cha upelelezi kinachoundwa na maofisa wa vyombo vya ulinzi na usalama kutoka makao makuu jijini Dar es Salaam tayari kimeanza kazi ya kuchunguza shughuli za uzalishaji na biashara ya madini ya almasi katika mgodi wa Mwadui unaomilikiwa na kampuni ya Williamson Diamonds Limited (WDL).
Kutokana na mahojiano yanayoendelea, shughuli za mgodi huo uliopo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga zimesimama kuanzia juzi kutoa fursa kwa viongozi na watumishi wa vitengo nyeti vinavyosimamia uchimbaji, uthamini na usafirishaji kuhojiwa.
Akizungumza kwa njia ya simu jana asubuhi, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Tellack alithibitisha uwapo wa kikosi kazi hicho mkoani humo na kufafanua kuwa shughuli za mgodi huo zitarejea kama kawaida baada ya mahojiano kukamilika.
“Hawajafunga mgodi. Kinachofanyika ni mahojiano na uchunguzi unaofanywa na maofisa wa ngazi za juu kutoka kwenye vyombo vya ulinzi na usalama. Yakikamilika shughuli zitarejea kama kawaida,” alisema Tellack.
Licha ya kuthibitisha uwepo wa kikosi kazi hicho mkoani mwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Simon Haule alisema hawezi kuzungumzia utendaji wake kwa sababu kinahusisha na kusimamiwa na maofisa kutoka makao makuu ya jeshi hilo jijini Dar es Salaam.
Bila kutaka kuingia kwa undani kuhusu suala hilo, Ofisa Uhusiano wa mgodi huo, Joseph Kaasa aliliambia Mwananchi kwa njia ya simu kuwa yuko kituo cha polisi na kuahidi kutoa taarifa atakapokamilisha kilichompeleka kituoni hapo.
WDL juzi ilisitisha kwa muda baadhi ya shughuli za uzalishaji mgodini, huku uongozi wa kampuni hiyo katika taarifa kwa wafanyakazi iliyotolewa Jumamosi kwa tangazo namba 3311 ukisema kwa mtazamo wa uchunguzi ulioanzishwa na Serikali na kwa sababu za kiusalama, umeamua kusitisha kwa muda baadhi ya shughuli za uzalishaji katika mgodi huo.
Taarifa hiyo ilisema shughuli ambazo zitaendelea ni za huduma maalumu za ulinzi, tiba, umeme, maji, zimamoto na usafiri unaohitajika katika huduma hizo.
“Huduma za kiutawala zitaendelea kufanya kazi. Tutawajulisha wakati uzalishaji utakaporejea,” ilisema taarifa ya kampuni hiyo.
WDL ilisema inasubiri kuachiwa kifurushi namba WI-FY18 cha almasi iliyokuwa ikisafirishwa nje kutoka mgodini.
Waziri wa Fedha, Philip Mpango akizungumza wakati alipopokea ripoti kuhusu shehena ya almasi iliyozuiliwa katika Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki alisema, “Tanzania ‘imepigwa vyakutosha’ hivyo wale wote waliohusika katika upigaji huo washughulikiwe.”

@ habari na mwananchi.co.tz

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...