DODOMA
Serikali imemshtaki John Hima (29) kwa kosa la
kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Namba 9 ya
mwaka 2015.
Akisoma kesi hiyo namba 9 ya mwaka 2018 katika
Mahakama ya Wilaya ya Bahi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Suniva Mwajumbe,
Inspekta Msaidizi Amani amesema kuwa mshtakiwa ametenda kosa hilo Januari 7
mwaka huu katika kijiji cha Nghulukano, Kata ya Chikola, Wilaya ya Bahi Mkoani
Dodoma.
Imeelezwa mahakamani hapo kuwa mshitakiwa ni
mwajiriwa wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) akiwa ni mkusanya taarifa
(mdadisi) katika Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi wa Mwaka
2017/2018 kwa Tanzania Bara.
Hata hivyo baada ya kusomewa mashtaka hayo, Mdadisi
Hima alikana mashitaka na kesi hiyo itasomwa tena tarehe 7 Februari, 2018
ambapo amerudishwa rumande baada ya kukosa wadhamini.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama,
Mwanasheria wa NBS Oscar Mangula amesema kuwa, mtuhumiwa Hima aliingia mkataba
na NBS kuwa mmoja wa wadadisi wa Utafiti huo unaoendelea hivi sasa ambao
ulianza Desemba mwaka jana.
Mwanasheria Mangula alieleza kuwa kesi hiyo
inawakumbusha wadadisi waliopewa jukumu la kukusanya taarifa za kitakwimu
kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa mikataba yao ya ajira, kiapo na mafunzo
waliyopewa ili kuepuka kutenda makossa ya kijinai kama analodaiwa kutenda na
mtuhumiwa.
Chanzo: Tanzania Today
#Changia Damu Okoa Taifa
No comments:
Post a Comment