Friday, 6 April 2018

MIMBA ZA UTOTONI ZAKATISHA NDOTO ZA WANAFUNZI 11 MPANDA



Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi imesema wanafunzi wapatao 11 katika shule zake wamepata ujauzito na kukatiza kuendelea na masomo.

Hali hiyo imebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Mpanda Michael Nzyungu wakati akiwasilisha taarifa kwa mkuu wa Mkoa wa Katavi kupitia kikao cha wadau wa elimu kilicholenga kujadili na kutathmini namna ya kuufanya mkoa wa Katavi ufanye vizuri katika mitihani ya taifa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Kwa upande wao baadhi ya wanafunzi na wadau wengine wamesema miongoni mwa vyanzo ambavyo bado vinasababisha mimba kwa wanafunzi walio na umri mdogo shuleni ni pamoja na malezi mabaya,umaskini pamoja na ukosefu wa mabweni hasa kwa watoto wa kike.

Hata hivyo serikali imekuwa ikiagiza kuchukuliwa hatua kali za kisheria dhidi ya wanaosababisha mimba kwa wazazi pamoja na wazazi au walezi wanaowaoza watoto wao kwa kigezo cha kupata mahali.

Mkoa wa Katavi ndiyo unaoongoza kwa mimba za utotoni kati ya mikoa ya Tanzania kwa kuwa na asilimia 45 ambapo wengi wao wanakuwa katika umri wa kuwa shuleni.

CHANZO:Isack Gerald 

No comments:

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...