Monday, 11 June 2018

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda




Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi na mwanamke ambaye hajafahamika majina wala makazi yake. 

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo,wamebainisha kuwa Kichanga hicho ambacho kinasadikiwa kimetupwa tangu majira ya jioni kimeokotwa majira ya saa kumi  alasiri. 

Wakizungumza na Mapanda Fm , mashuhuda hao wamesikitishwa na kitendo hicho huku wakiomba hatua kali zichukuliwe dhidi ya mwanamke atakayebainika kutenda unyama huo. 

Afisa Ustawi wa jamii manispaa Redgunda Mayolwa ameiomba jamii kutoa ushirikiano kwa viongozi wa serikali na jeshi la Polisi ambao wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo,na kumbaini mwanamke aliyetenda tukio hilo la kinyama na kusema kwamba kitendo cha kutupa mtoto hakina tija kwa jamii. 

Jamii imeshauriwa kutoa ushirikiano  kwa viongozi wa ngazi zote ikiwemo Jeshi la Polisi Ili kuweza kuyakomesha matukio hayo


Sunday, 10 June 2018

DC MUHANDO AWACHARUKIA WANAOISHI MAENEO YASIYO RASIM KATIKA WILAYA YAKE


Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Salehe Muhando amewataka wakazi wanaoishi katika maeneo yasiyo rasmi kwa makazi yakiwemo Kalumbi,Migengebe na Kidongo Chekundu kuondoka katika maeneo hayo kabla ya Julai 18 mwaka huu.

Muhando ametoa wito huo katika ziara ambayo ameifanya katika kata ya Katuma kwa ajili ya kuelimisha wananchi katika masuala mbalimbali ikiwemo utunzaji wa mazingira katika msitu wa Tongwe Magharibi unaozungukwa na vijiji 11 kati ya 55 vya wilaya hiyo.

Aidha Muhando amemwagiza Mkuu wa Kituo cha Polisi Kata Katuma Chilongo Fwele,kuwakamata wananchi wanaoendelea kuharibu chanzo cha maji cha mto Katuma kwa kufanya shughuli za kibinadamu zinazokiuka umbali wa mita 60 kutoka chanzo cha mto
Hata hivyo baadhi ya viongozi wa kata ya Katuma wameshauri udhibiti wa watu wanaoharibu mto Katuma ufanyike kwa maeneo yote yanayozunguka mto huo.

Saturday, 9 June 2018

SEKONDARI YA MWANGAZA YAKABILIWA NA UHABA WA MTAALAM WA MAABARA


Na;Neema Husein 
Shule ya sekondari Mwangaza iliyopo Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi inakabiliwa na changamoto mtaalam wa maswala ya maabara licha  ya kuwepo na vifaa vya kutosha.

Hayo yamebainishwa na mkuu wa shule hiyo Simeon Lubange wakati akizungumza na Mpanda Radio ofisini kwake na kusema kuwa walimu wa masomo ya sayansi inawaradhimu kuchukua jukumu la mtaalam huyo.

Aidha amewataka wanafunzi wa shule hiyo kutumia fursa  vizuri ya kuwepo kwa maabara ya masomo matatu ya sayansi  shuleni hapo.

Hata hivyo ameiomba serikali kutatua tatizo hilo mapema kwa kuleta wataalam wa maswala ya maabara katika shule ambazo hazina wataalam hao.

JITOKEZENI KUSHIRIKI MIRADI YA JAMII-DC MATINGA


Na;Restuta Nyondo 
Wananchi wa Wilaya ya Mpanda wametakiwa kujitoa katika kushiriki katika kuchangia miradi mbali mbali ya maendeleo hususani sekta ya elimu na afya.

Mkuu wa wilaya ya Mpanda Lilian Charles Matinga akizungumza na Mpanda radio ofisin kwake Amesema kuwa mwamko wa wananchi katika kuchangia maendeleo bado ni mdogo hali inayopelekea kuchelewesha maendeleo.

Matinga  ametoa wito kwa wazazi kujitoa katika kuchangia chakula mashuleni ili kuboresha afya za wanafunzi na kuongeza ufanisi katika taaluma.

Ni wajibu wa mwananchi kuchangia asilimia 20 ya maendeleo na serikali kuchangia asilimia 80.

WANANCHI MANISPAA YA MPANDA WALALAMIKIA ZOEZI LA VITAMBULISHO VYA TAIFA


Na;Rebeka Kijja
Baadhi ya wananchi katika Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi wamelalamikia utaratibu uliowekwa katika zoezi la kujiandikisha vitambulisho vya uraia.

Wamesema hayo wakati wakizungumza na Mpanda Radio kwa nyakati tofauti ambapo wameeleza kuwa maelezo wanayopewa na wasimamizi wa zoezi hilo bado hayajakidhi uhitaji wao hali ambayo inawafanya waone ugumu katika kukamilisha zoezi.

Katika hatua nyingine wazee na watu wenye ulemavu wameiomba serikali kuwaangalia kwa ukaribu kwani zoezi kwao linakuwa gumu hali inayowafanya wajione kama wametengwa katika zoezi hilo.

Wazo la kuanzisha Vitambulisho vya Taifa kwa raia wa Tanzania na wageni waishio nchini Tanzania lilizaliwa mwaka 1968 katika kikao cha “Interstate Intelligence Gathering” kilichojumuisha wajumbe Kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Uganda na Zambia ambapo iliazimiwa kwamba ili kuimarisha mahusiano ya kiusalama yanayozingatia Utawala wa Sheria katika nchi hizo nne

MANISPAA YA MPANDA YAWATIMUA WAOSHA MAGARI MTO MPANDA


Na:Haruna Juma 
Baadhi ya vijana waliokuwa wakiosha magari katika Mto mpanda eneo la Misunkumilo wameiomba Manispaa ya Mpanda kuwatengea eneo lingine la kufanyia shughuli hiyo baada ya kuwatimua kutoka Mto huo.

Wakizungumza na mpanda Radio vijana hao wamesema kwa muda mrefu sasa vijana wengi wamekuwa wakijipatia riziki kutokana na shughuli hiyo

Wamesema uongozi wa manispaa ulipaswa kutafuta mbinu mbadala ya kuwaondoa mtoni badala ya njia iliyotumika ambayo wamesema inaweza kuleta madhara kwa jamii nzima.

Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda imepiga marufuku shughuli za kuosha magari katika vyanzo vya maji ili kutunza mazingira na vyanzo vya maji



VIBOKO WAZIDI KUZUA HOFU KWA WAKAZI WA KATUMA


Wakazi wa kata ya Katuma Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi,wameiomba serikali kuwaondoa viboko katika makazi ya watu

Wakizungumza katika Mkutano wa hadhara katika kijiji cha Katuma wamesema  kwa sasa viboko wanazagaa maeneo ya Zahanati ya Katuma na kula mazao shambani

Kaimu Afisa ardhi na maliasli wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda Bw.Elisha Mengele,amekiri kupata taarifa za kuzagaa wanyama hao kutoka mto Katuma na kuwataka wananchi kutoa taarifa sahihi na  ushirikiano

Wakazi wa wilaya ya Tanganyika na Mpanda wanaozunguka mto Katuma wamkuwa wakilalamika mazao yao kuvamiwa na viboko hao ambapo kwa mjibu wa Bw.Mengele viboko huhama katika maeneo yao msimu wa masika.

Thursday, 7 June 2018

RASMI MSITU WA TONGWE MIKONONI MWA WILAYA YA MPANDA-DC MUHANDO

Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi Salehe Muhando,amesema wizara ya maliasili na utalii imekubali msitu wa Tongwe Magharibi kumilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda kutoka katika mamlaka ya wizara hiyo.

Muhando amebainisha hatua hiyo kupitia mikutano ya hadhara katika vijiji vya Kapanga na Katuma Kata ya Katuma lengo likiwa ni kuelimisha kutunza msitu huo wenye zaidi ya sokwe 800 kwa ajili ya faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda Mh.Hamadi Mapengo amesema mchakato wa kuomba kumiliki msitu huo ulianza mwaka 2002 ambapo kwa sasa kutaongezeka mapatao yatokanayo na msitu ikiwa ni pamoja na kupata watalii kwa ajili ya kuja kuwaona wanyama.

Kwa mjibu wa Kaimu wa afisa ardhi na maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda Bw.Elisha Mengele,vijiji vipatavyo 11 vinavyozunguka msitu huo vikiwemo Kapanga,Lugonesi,Katuma,Mpembe na Tongwe vinatarajia kunufaika zaidi na msitu huo.


WAZALISHAJI ASALI KATAVI TUMIENI NEMBO YA TBS KUINUA UBORA WA BIDHAA ZENU-MARANDU


Wajasiriamali wanaojishughulisha  na uzalishaji wa Asali katika mkoa wa Katavi wameshauriwa kuzalisha bidhaa hiyo kwa kuzingatia uwekaji wa alama Tambuzi yaani bakodi na kwa kuzingatia  viwango vinavyo tambuliwa na shirika la kudhibiti ubora wa bidhaa Tbs.

Hayo yamebainishwa na kaimu katibu Tawala mkoa wa Katavi Wilbad Marandu wakati akifungua semina ya wazalishaji wa bidhaa hiyo yanaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Idara ya maji manispaa ya Mpanda.

Pia amesema bidhaa nyingi zitokanazo na nyuki zimekuwa zikizalishwa pasipo kuwekewa alama Tambuzi hali ambayo huwakosesha fursa ya bidhaa hiyo kuuzika kimataifa.


Kwa upande wake mwakilishi wa shilika la kizibiti ubora wa bidhaa Tanzania tbs kutoka mikoa ya nyanda za juu kusini Abeli  Clement amaesema jukumu kubwa la la shilika hilo nikuhakikisha bidhaa zinazo zalishwa zipo katika kiwango kinacho kubalika.

TUNZENI MIRADI YA MWENGE-DC MATINGA


Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Lilian Charles Matinga amewataka wananchi kutunza miradi ya maji ambayo imezinduliwa na mwenge wa uhuru ili iweze kutumika kwa malengo husika.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na Mpanda Radio ofosini kwake na kusema kuwa miradi iliyozinduliwa yote imeshaanza kutumika hususani miradi ya visima vya maji na kuwataka wananchi kuunda kamati za maji ili kuindeleza miradi hiyo.

Aidha amesema kuwa utunzaji wa miundominu ni  wajibu wa jamii nzima ikisimamiwa na kamati ya watumia maji.

Mei 2 mwaka huu Mwenge wa uhuru katika halmashauri ya manspaa ya Mpanda ulizindua miradi 10 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi milioni 800 ikiwemo miradi ya Kisima cha maji,zahanati ya Milala,klabu za kupambana na rushwa,mimba za utotoni pamoja na madawa ya kulevya.

JESHI LA POLISI MKOANI KATAVI LAAPA KULA SAHANI MOJA NA MATAPELI KWA NJIA YA MTANDAO



Jeshi la Polisi mkoani Katavi limewataka wananchi kutoa tarifa ya vitendo vya utapeli kwa njia ya simu za mkononi.

Hayo yamesemwa na kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Katavi Benedict  Mapugila alipokuwa akihojiwa kwa njia ya simu mapema leo, ambapo amekili kuwepo kwa vitendo hivyo, na kuwataka wananchi kutofuata  maelekezo yanayotolewa na matapeli kwanjia ya ujumbe mfupi.

Kuenea kwa ujumbe huo ambao hutoa maelekezo namna ya  kutuma fedha kwenye namba nyingine  ambayo huambatanishwa kumezua hofu kubwa miongoni mwa jamii, huku wangine wakikosoa kuhusu udahifu wa mitandao hiyo juu ya kupambana na suala hilo.

Nisiku moja tu tangu msemaji wa Jeshi la polisi nchini Barnabas Mwakalukwa kuutadharisha umma juu ya vitendo hivyo.

Wednesday, 6 June 2018

RTO KATAVI APIGA MARUFUKU MAGARI MABOVU KUSAFIRISHA ABIRIA


Wamiliki  wa magari wametakiwa kutoruhusu magari mabovu ya safari za mikoni kuingia mkoani katavi kutoa huduma ya usafiri.

Mkuu wa polisi kikosi cha usalama  barabarani  mkoa wa katavi willy Joas Mwamasika  amesema hayo wakati akizungumza na Mpanda Redio na kusema kuwa baadhi yao wamekuwa wakiufanya mkoa wa katavi kama dampo la magari mabovu.

Amesema watu wamekuwa wakikiuka sheria za usalama barabarani kutokana na mazoea yaliyokuwepo tangu mwanzo hivyo kutokana na oparesheni ya nyakuanyakua itaondoa mazoea hayo.

Hivi karibuni Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Fortunatus Musilimu, amesema dereva yeyote wa mabasi yaendayo mikoani anayeshindwa kufuata sheria na alama za barabarani ni vyema akaacha kufanya kazi hiyo kwa kuwa atakamatwa kwa mtindo wa ‘nyakua nyakua’.

JESHI LA POLISI KATAVI LABARIKI KUSHIRIKIANA NA JAMII,KUANZA KWA ULINZI SHIRIKISHI


Ulinzi wa polisi jamii na ulinzi shirikishi katika kata ya Majengo Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi,Umeanza baada ya taratibu za kuunda vikundi kukamilika.

Katika Mahojiano na Mpanda Radio,Mkuu wa kituo cha polisi Wilaya ya Mpanda Milton Sandari amesema tayari vikundi katika mitaa ya Majengo,Mji mwema na Maridadi vimeandaliwa.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Majengo John Salanda ameiambia Mpanda Radio kuwa wao tayari wametekeleza agizo la Kamanda Nyanda la kuwataka kuandaa Ofisi kwa ajili ya Polisi Kata ambapo amesema mpaka sasa hajaletwa.

Mei 25 mwaka huu,kamanda Nyanda kupitia mkutano wa hadhara katika kata ya Majengo,alimwagiza Mkuu wa polisi kituo cha Polisi wilaya ya Mpanda Milton Sandari kuhakikisha vikundi vya ulinzi shirikishi vinaundwa haraka ili kudhibiti uhalifu uliopo katika kata hiyo.

WAFANYABISHARA MPANDA WALIANA NA ZOEZI LA UGAWAJI WA LESENI


Wafanyabiashara katika soko kuu Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi wamesema utaratibu uliowekwa wa kupata leseni ni changamoto katika kukamilisha masharti ya kufanya biashara.

Wakizungumza na Mpanda Radio kwa nyakati tofauti wamesema wafanya biashara wengi wanashindwa kupata leseni hizo kwa wakati kutokana na usumbufu wanaoupata katika mchakato wa upatikanaji wa leseni hizo.

Hata hivyo wameiomba serikali kuwapa muda wafanya biashara ili elimu ili kila mfanyabiashara aweze kutambua umuhimu wa kulipia leseni hizo.

Hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Liliani Charles Matinga alimpa wiki moja Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda kuhakikisha kila mfanyabihashara anakuwa na leseni.

Tuesday, 5 June 2018

WAFANYABIASHARA MKOANI KATAVI WALIA NA MKWAMO WA BIASHARA KUTOKANA NA ONGEZEKO LA KODI



Jumuiya ya wafanyabiashara mkoa wa Katavi imesema kuna mkwamo mkubwa wa kibiashara nchini kutokana na  kuongezeka kwa kodi na tozo mbali mbali.

Hayo yameelezwa na mwenyekiti wa Jumuiya hiyo mkoani Katavi Aman Mahelah alipokuwa akizungumza na Mpanda radio amesema suala la kutetea maslahi ya wafanya biashara limekwamishwa na kukosekana kwa uelewa wa pamoja kati ya serikali na wafanyabishara.

Pamoja na hayo amezitaja baadhi ya changamoto zinazo ikabili jumuia hiyo kushindwa kupata majibu sahihi kutoka serikalini ambapo baadhi ya watendaji wa serikali  hugeuzwa madai  hayo kuwa ni ya wapinga maendeleo na wakwepa kodi 

Jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania ilianzishwa kwa nia ya kutetea maslahi ya wafanya biashara na kutatua changamoto zinazo ikabili sekta  ya biashara.




JIANDAENI NA MSIMU MPYA WA MAUZO YA PAMBA-DC TANGANYIKA


Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi  Swalehe Mbwana Muhando amewataka wakulima wa zao la Pamba wilayani humo kujiandaa na msimu wa mauzo .

Muhando ametoa Kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari na kufafanua kuwa  serikali inaendelea na utaratibu wa awali ili kutangaza rasmi tarehe ya ununuzi.

Katika hatua nyingine amezionya baadhi ya kampuni zinazo jihusisha na ununuzi wa zao hilo kuachana na vitendo vya udanganyifu kwenye vipimo vinavyo tumika.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Mkoa wa Katavi kuuza pamba tangu kuanzishwa kwa makakati wa kilimo cha mazao mbadala kama vile korosho,alizeti na Pamba.

Friday, 1 June 2018

UPIMAJI UKIMWI NYUMBA KWA NYUMBA



Wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda wametoa maoni toafauti juu ya kuanzishwa kwa kampeni ya upimaji  wa virusi vya ukimwi nyumba kwa nyumba.

Wakizungumza na Mpanda Radio wamesema kuwa kampeni hiyo itasaidia katika kupunguza maambukizi mapya ya ugonjwa huo na kuongeza uelewa wa wananchi waliokuwa na hofu ya kupima virusi  vya ukimwi.

Aidha wametaja sababu za wanaume wengi kutokuwa tayari kupima kuwa ni pamoja na uoga kutokana na wengi wao hujikuta katika wimbi la ngono isiyo salama.

Kwa mujibu wa  Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Serikali imeandaa kampeni maalum ya kuhamasisha upimaji wa VVU na kuanza matumizi ya dawa za kufubaza VVU mara moja  hususani  kwa wanaumena na SS Kampeni hiyo inatarajiwa kuzinduliwa jijini Dodoma tarehe 19 Juni mwaka huu.
CHANZO:Restuta Nyondo

WAZAZI WAMETAKIWA KUWA MSTARI WA MBELEE KATIKA MASWALA YA ELIMU


Wazazi wametakiwa kuacha tabia ya kuwashawishi watoto wao kufanya vibaya katika mitihani kwa lengo la kuwaozesha ili wapate mahari.

Kauli hiyo ameitoa mkuu wa wilaya ya Tanganyika Salehe Mhando ambapo amesema wazazi wamekuwa wakichangia kwa kiasi kikubwa kurudisha Maendeleo ya wanafunzi nyuma hususani wanafunzi katika shule za msingi.

Mhando amesema kila mmoja anawajibu wa kuhakikisha anashiriki katika kuinua elimu ili wanafunzi wafikie ndoto zao hivyo hatua kali zitachukuliwa kwa wazazi ambao watabainika kuwakatisha wanafunzi masomo.

Kwa mujibu wa Takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, wasichana 8000 kila mwaka huacha shule kutokana na ujauzito na  Kati yao 3,000 ni wanafunzi wa shule za msingi.
 CHANZO:Rebecca Kija

WAFUGAJI KATAVI KUANZA MCHAKATO WA CHAMA CHA USHIRIKA


Wafugaji Mkoani Katavi  wameanzisha mpango wa kuwepo kwa chama cha ushirika cha wafugaji kitakacho kuwa na uwezo wa kutatua changamoto za wafugaji  .

Wakizungumza katika kikao cha mchakato huo katika ukumbi wa mikutano wa galden wamesema kuanzishwa kwa ushirika huo  kutawasaidia  watambulike  kisheria

Mwenyekiti wa wafugaji  mkoa wa Katavi Mussa Kabushi amesema umoja huo utawaunganisha  pamoja na kurahisisha  upatiakaji wa masoko kwa mifugo .

Mkoa wa Katavi  unatajwa kuwa na idadi kubwa ya wafugaji sambamba na shughuli za kilimo kutokana na jiografia ya mkoa.
CHANZO:Paul Mathius

KUENDELEZA AMANI KATIKA MWEZI MTUKUFU



Waislamu mkoani Katavi wameaswa kudumisha ibada ndani ya  mwezi mtukufu wa radhani kwa Uadilifu uaminifu na unyenyekevu.

Amani Rajabu Athuman ni katibu wa baraza la waislamu mkoani katavi amesema  mwezi mtukufu wa ramadhani unazidisha malipo mara dufu kama mwislamu atatimiza ibaada.

Ibada ya funga ni ibada kwa watu wenye afya ambao wanatakiwa kushinda bila ya kula na Watu wanaoruhusiwa kula mchana katika mwezi wa Ramadhani ni watoto, wanawake wajawazito, wagonjwa na wanawake ambao wamo katika mzunguko wa hedhi.

Leo ni Ramadhani ya 17 tangu kuanza kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhani.
CHANZO:HARUNA JUMA

Featured post

MASIKINI WEEE!!!!! KICHANGA CHA SIKU MOJA CHAOKOTWA KATIKA KIWANJA CHA MPIRA AZIMIO

Na;Ezelina Yuda Mtoto mchanga mwenye jinsia ya Kike anayekadiriwa kuwa wa siku 1 ameokotwa akiwa hai kandokando ya uwanja wa azimio  ...